1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake sharti wapewe ulinzi

Thelma Mwadzaya25 Novemba 2008

Kila mwaka siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake huadhimishwa tarehe 25 mwezi Novemba.Maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 1981 baada ya mauaji katili yaliyowasibu ndugu watatu wa kike

https://p.dw.com/p/G1UQ
Navi(Navanethem) Pillay Kamishna wa masuala ya haki za binadamu katika Umoja wa MataifaPicha: AP


Wanawake hao walikuwa wanaharakati wa kisiasa katika Jamhuri ya Dominica na waliuawa kikatili tarehe hiyo baada uongozi wa wakati huo kutoa agizo hilo.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito wa msukumo zaidi kutolewa ili kupambana na ukatili.


Mwezi Februari mwaka huu Bwana Ban Ki Moon alianzisha kampeni maalum itakayoendelea hadi mwaka 2015 inayowahamasisha wadau wote kuungana ili kupambana na ukatili dhidi ya wanawake.Mwezi Juni mwaka huu huu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa upande wake liliidhinisha azimio 1820 linalotambua ukatili wa kijinsia katika mazingira ya vita jambo linaloathiri juhudi za kudumisha amani na usalama.Chini ya azimio hilo wahusika wote katika vita wana jukumu la kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wa kike wanalindwa.


Katika taarifa yake ya maadhimisho ya siku hii Kamishna wa masuala ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Bi Navi Pillay ameeleza kuwa ukatili dhidi ya wanawake katika maeneo yanayozongwa na vita umekithiri.Alitolea mfano Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo ambako eneo la mashariki mwa nchi hiyo linakabiliwa na vita vya mara kwa mara kati ya waasi na wanajeshi wa serikali.Kwa mujibu wa takwimu wanawake wengi na watoto wamebakwa,kupigwa,kufanyiwa ukatili,kukamatwa na kuzuiliwa bila hiari na hata kuuawa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.Hata hivyo hakuna mhusika yoyote aliyechukuliwa hatua za kisheria au kuadhibiwa.Baadhi ya wanawake wa eneo la mashariki ya Kongo nao wanaafiki hilo.


Katika nchi jirani ya Rwanda mfuko maalum wa Umoja wa mataifa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ulifadhili mradi wa kutoa mafunzo maalum kwa wanawake waliokuwa katika mstari wa mbele kwenye vita.Wengi ya wanawake hao wanaripotiwa kuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia wakati vita vilipoendelea nchini humo.Rwanda iligubikwa na mauaji ya halaiki mwaka 1994 ambapo zaidi ya watu laki nane walipoteza maisha yao katika kipindi cha siku 100.


Mradi huo uliwapa wanawake fursa na jukwaa salama la kuelezea yaliyowasibu wakati wa vita.Kadhalika mpango huo uliwawezesha kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia pamoja na ugonjwa wa Ukimwi katika jamii.


Bi Pillay aliye pia mwanasheria alisisitiza kuwa ukatili dhidi ya wanawake unatokea hata katika maisha ya kila siku katika baadhi ya mataifa ambako mila na tamaduni zinamnyanyasa mwanamke.


Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO majeraha wanayoyapata wanawake wanaofanyiwa ukatili na waume wao yana athari za muda mrefu pia.Utafiti wa shirika hilo ulibaini kuwa vitendo vya ukatili vinasababisha matatizo wakati wa uja uzito,sehemu za siri za kike,tumboni na maumivu kwa jumla.

Tathmini hiyo inafafanua kuwa wanawake ambao wamefanyiwa ukatili wa aina moja au nyingine wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na mawazo ya kutaka kujiua vilevile kujaribu kumaliza maisha yao.

Kampeni iliyoanzishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ni kielelezo cha hatua za ushirikiano katika vita dhidi ya ukatili kwa wanawake hadi ifikapo mwaka 2015.Huo ndio muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa wa kutimiza malengo ya maendeleo ya Millenia.