1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kupambana na umaskini duniani

Grace Kabogo
17 Oktoba 2017

Tarehe 17 Oktoba ni siku ya kupambana na umaskini duniani, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa inasema ''Njia ya kuelekea jamii zenye amani na umoja''.

https://p.dw.com/p/2lxba
Bangladesch Kinderarbeit in Dhaka
Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Hasan

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, siku ya kupambana na umaskini inaadhimishwa kwa kuzingatia wito uliotolewa miaka 25 iliyopita ya kutambua ujuzi na ujasiri wa familia zinazoishi katika umaskini duniani kote, umuhimu wa kuwafikia zaidi maskini na kuanzisha ushirikiano na wananchi wanaotoka katika mazingira yaliyokuwa na umaskini na wenye nia ya kuutokomeza umaskini.

Wito huo ulichukuliwa na kufanyiwa kazi katika nchi nyingi duniani na umewawezesha watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kuvunja ukimya na kuzungumza kuhusu umaskini pamoja na kuchukua hatua katika kushirikiana na wale wanaotamani kuwa washirika wao. Kaulimbiu ya mwaka huu inakumbushia umuhimu wa maadili ya heshima, mshikamano na kuwa na sauti moja katika kuitikia wito wa kuutokomeza umaskini kila mahali.

Maadili hayo pia yanaonekana katika ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, ambayo yameliweka suala la kupambana na umaskini kama lengo kuu na kuzilazimisha nchi zote kuutokomeza umaskini katika mifumo yote, kupitia mikakati inayohakikisha kwamba inatimiza haki zote za binadamu na kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema aina nyingi za umaskini zinasababishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira, kukosekana kwa usalama na usawa, mizozo na mabadiliko ya tabia nchi.

Watu milioni 800 duniani wanaishi na umaskini

''Leo tunaungana na watu milioni 800 duniani wanaoishi katika umaskini uliokithiri. Lakini tumepiga hatua katika kuondoa umaskini tangu 1990 na nchi zote zimejizatiti katika kuutokomeza umaskini. Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu inaahidi kuhakikisha dunia yenye afya, salama na kujenga jamii iliyo na amani na umoja unaoheshimikwa kwa wote,'' alisema Guterres.

Russland St. Petersburg International Economic Forum Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN, Antonio GuterresPicha: Reuters/S. Karpukhin

Umuhimu wa uelewa wa umma, sauti ya pamoja na kuwashirikisha ipasavyo watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri, unatambuliwa katika ajenda yenyewe na kwenye mchakato wa mashauriano yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba uwajibikaji na vipaumbele vya mamilioni ya watu, hasa wale wanaoishi katika umaskini uliokithiri, wanajumuishwa na kusikilizwa. Kushirikishwa ipasavyo kwa watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kampeni ya kimataifa pia inawakaribisha watu binafsi, jumuiya, mashirika na nchi mbalimbali kuiadhimisha siku hii katika njia tofauti, ikiwemo kugundua au kuelezana jinsi umaskini unaweza ukatokomezwa, wakati watu wanapoungana pamoja katika juhudi za kuimarisha haki kwa wote.

Mwaka huu pia ni kumbukumbu ya miaka 30 ya Siku ya Kuushinda Umaskini Uliokithiri Duniani. Siku hii ilitambuliwa na Umoja wa Mataifa baada ya wito uliotolewa na Padre Joseph Wresinski. Oktoba 17, 1987, watetezi wa haki za binaadamu na haki za kiraia kutoka duniani kote walikutana mjini Paris, Ufaransa kwa lengo la kuahidi kuonyesha mshikamano na watu wote ulimwenguni na kujitahidi kuondoa umaskini uliokithiri.

Kwa mujibu wa mkutano huo uliohudhuriwa na zaidi ya watu 100,000, ''Pindi wanaume na wanawake wakiishi katika umaskini uliokithiri, haki za binaadamu zinakiukwa.'' Wanaharakati hao wanasema waliungana pamoja kuhakikisha haki hizo zinaheshimiwa, kwani huo ni wajibu wao. Mafanikio ya ulimwengu usio na umaskini, yanatoa mwelekeo wa kuzifikia jamii zenye amani na umoja kama ilivyoandikwa kwenye Lengo la 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/http://bit.ly/1Ccqf8F
Mhariri: Daniel Gakuba