1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Maji Duniani

P.Martin22 Machi 2007

Tangu mwaka 1993,tarehe 22 mwezi Machi huadhimishwa kama ni Siku ya Maji Duniani.Lengo la siku hii ni kusisitiza matatizo yanayohusika na bidhaa hii yenye thamani.

https://p.dw.com/p/CHlP

Mada ya mwaka huu ni upungufu wa maji,hasa wakati huu ambapo athari za ongezeko la joto duniani zimeanza kudhihirika.

Wajumbe wa Baraza la Maji Duniani walipokutana juma hili mjini Brussels,walitoa wito kutambua kuwa maji ni haki ya kimsingi ya kila binadamu na yasidhibitiwe na mashirika ya kibinafsi.Waziri wa maji wa Bolivia akisisitiza haki hiyo amesema, kila mmoja wetu ana haki ya kujipatia maji bila ya upingamizi,kwani maji ni uhai wa binadamu. Itambuliwe kuwa maji ni haki ya binadamu.

Wakati huo huo mkuu wa WHO-Shirika la Afya Duniani,Dr.Margaret Chan amesisitiza uhusiano uliopo kati ya afya na hakika ya kupata maji yalio safi.Bibi Chan akaeleza kuwa kila mwaka, zaidi ya watu milioni 1.6 hufariki kwa sababu hawana njia ya kujipatia maji yalio safi.Asilimia tisini ya vifo hivyo ni vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na hasa hutokea katika nchi zinazoendelea.Kwa maoni yake,hivyo ni vifo vinavyoweza kuepukwa kwa kuwa na utaratibu bora wa kusimamia ugawaji wa maji na kupunguza uambukizaji wa malaria na magonjwa mengine.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,ifikapo mwaka 2025,theluthi mbili ya binadamu humu duniani, watakabiliwa na matataizo ya maji.Nchi zitakazoathirika vibaya zaidi ni zile za barani Afrika,Mashariki ya Kati na Asia ya Magharibi.

Kwa mfano hivi sasa nchini Chad,kwa sababu ya idadi kubwa ya binadamu wanaovua katika Ziwa Chad na wanaotumia maji ya ziwa hilo kumwagilia mashamba yao,kima cha maji katika ziwa hilo kimepunguka kwa mita tano.

Wataalamu wanaonya kuwa ongezeko la joto duniani litazidi kuathiri vibaya sana akiba ya maji.Ni dhahiri kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanazidi kuwa kitisho,wakati ambapo mafuriko na ukame huhatarisha uwezo wa kuwa na maji yalio safi na hivyo maradhi kama kipindupindu,homa ya matumbo na malaria huongezeka.

Wakati huo huo,maafisa wa Baraza la Maji Duniani,ambao ni kutoka jamii za kiraia na mashirika yasio ya kiserikali,wamesisitiza wasiwasi wao kuwa maji yanazidi kuwa chanzo cha migogoro ya mikakati na uchumi.Kwa maoni ya wajumbe hao,hatua lazima zichukuliwe kuhakikisha kuwa maji duniani yanadhibitiwa na jamii na sio mashirika binafsi ya biashara.Sasa ndio Baraza la Maji Duniani linapanga kuwasilisha barua kwa viongozi wa serikali na katika Umoja wa Mataifa, kuwasadikisha viongozi hao umuhimu wa kuwepo haki mpya ya binadamu kuhusika na maji.