1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Mtoto wa Afrika yaadhimishwa

16 Juni 2011

Leo ni siku ya kimataifa ya kumkumbuka mtoto wa Kiafrika, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Kwa pamoja, tunaweza kulitafutia suluhu tatizo la watoto wanaorandaranda mitaani", hukuwa watoto milioni 50 wakiwa mayatima.

https://p.dw.com/p/11bsk
Watoto wa Kiafrika
Watoto wa KiafrikaPicha: AP

Pamoja na kutaja idadi ya watoto hao waliojikuta mayatima, wengi wao kutokana na janga la Ukimwi, ripoti ya mwaka huu ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF) inaeleza kwa kina zaidi kuwa idadi kubwa ya watoto wanaofanyishwa kazi kwa lazima wako katika eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara.

Takwimu zinaeleza kuwa zaidi ya thuluthi moja ya watoto hao wana umri ulio kati ya miaka 5 hadi 14 na wanafanyishwa kazi ngumu.

Kulingana na UNICEF, katika bara hilo hilo la Afrika, maelfu ya watoto wanateswa, kutumiwa vibaya pamoja na kufanyiwa ukatili. Shirika hilo linazitolea wito serikali kuziongeza juhudi zao za kuyalinda maslahi ya watoto.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UNICEF, Anthony Lake, anasisitiza kuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wako katika hatari zaidi.

"Tunajua kwamba, tukizikita juhudi zetu kuyaangazia matatizo ya familia zilizo na mahitaji mengi zaidi, na kuzifikia jamii ziilizoko kwenye maeneo ya mbali tunaweza kufanikiwa. Hii ni kwa sababu tunahitaji kuliimarisha hili vuguvugu la kuhakikisha kuwa tunayatilia maanani maslahi ya watoto." Anasema Lake.

Mtoto wa kike wa Kitanzania akitafuta maji
Mtoto wa kike wa Kitanzania akitafuta majiPicha: Christoph Gödan

Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNICEF amesisitiza pia kuwa kuna umuhimu wa kila mmoja kufanya kila awezalo kila siku kuijua sababu na kiini cha watoto kutengwa na wazazi wao. Alifahamisha kuwa kuna haja ya kuwa na ari mpya ya kuwalinda watoto kokote waliko.

Shirika la UNICEF linazitolea wito serikali kuiimarisha mifumo yake ya kuwasaidia watoto kwa minajili ya kuhakikisha kuwa wana usalama wa kutosha na pia wanapata huduma muhimu katika jamii.

Shirika hilo linaeleza pia kuwa umasikini uliokithiri, mizozo, athari za ugonjwa wa Ukimwi pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na purukushani nyumbani, ni mambo yenye mchango mkubwa katika suala zima la watoto kukimbia majumbani mwao na kuangukia mitaani.

Hali hiyo inawaweka katika hatari na kuuongeza uwezekano wa kunyanyaswa zaidi. Eneo la Karamoja la Uganda linakabiliwa na tatizo la watoto kurandaranda mitaani kwa sababu ya hali ngumu ya maisha na ghasia. Ili kulitafutia suluhu jambo hilo, serikali ya Uganda ilianzisha mpango maalum, ikiwemo kumteua waziri maalum anayeshughulikia masuala ya eneo hilo, ambaye kwa sasa ni Barbara Nekesa Oundo.

Bi Oundo anasema kuwa kuna vyanzo vingi vya tatizo la watoto na wanawake kukimbilia maeneo ya mjini. "Kwa hiyo tunaporejea hapa na kuyatafutia suluhu matatizo yaliyopo kwenye eneo hili, inakuwa rahisi zaidi kuwarai warejee nyumbani".

Ripoti hiyo ya UNICEF inaeleza kuwa kiasi ya watoto milioni 15 ni mayatima kwa sababu ya maafa yanayosababishwa na ugonjwa wa Ukimwi.

Eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara linaripotiwa pia kuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto wanaofanyishwa kazi ngumu na hatari.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya/DPAE/UNICEF Multimedia
Mhariri: Saumu Mwasimba