1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya mtoto wa kike duniani

Admin.WagnerD11 Oktoba 2012

Leo (11.10.2012) ni siku ya kimataifa ya mtoto wa kike. Dunia inaadhimisha siku hii wakati kukiwa na changamoto nyingi zinazomuandama mtoto wa kike ikiwemo kunyimwa fursa ya kupata elimu na haki zake nyinginezo.

https://p.dw.com/p/16Nl8
Malala Yousafzai
Malala YousafzaiPicha: picture-alliance/dpa

Nchini Pakistan msichana aliyepigwa risasi na kundi la Taliban kwa kupigania haki yake ya kupata elimu, afya yake imeimarika kiasi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kuwaoza watoto wa kike mapema ndio ukiukaji mkubwa wa haki za binadaamu wanaofanyiwa wasichana katika mataifa mbalimbali.

Malala akipata matibabu hospitalini
Malala Yousafzai akipata matibabu hospitaliniPicha: picture-alliance/dpa

Katika tamko lililotolewa leo kwenye maadhimisho ya siku hii, Umoja wa Mataifa umesema kuwa hali ni mbaya zaidi nchini Afghanistan ambapo nusu ya wasichana wanaozwa chini ya umri wa miaka 18 huku mmoja kati ya watoto sita walioozwa akiwa chini ya miaka 15.

Madhara ya kuwaoza watoto mapema

Kuwaoza watoto chini ya umri ndio sababu kubwa inayochangia katika vifo vya akinamama na watoto nchini Afghanistan ambapo katika kila vizazi 100,000 vifo 327 hutokea na vingi vinawahusu watoto wa kike wenye umri wa miaka 10 hadi 14.

Umoja wa Mataifa unalinyooshea kidole kundi la wanamgambo wenye msimamo mkali wa kiislamu la Taliban kuhusika kwa kiasi kikubwa na madhara hayo wanayoyapata watoto wa kike nchini humo.

Kundi la wanamgambo wa Taliban nchini Pakistan
Kundi la wanamgambo wa Taliban nchini PakistanPicha: AP

Chini ya utawala wa Taliban nchini humo katika kipindi cha mwaka 1996 hadi 2001 watoto wa kike hawakuruhusiwa kupata elimu.

Mashambulizi dhidi msichana wa Pakistan

Kundi hilo hilo la Taliban ndilo linalohusika na shambulizi dhidi ya msichana Malala Yousafzai mwenye umri wa miaka 14 ambaye alipigwa risasi akiwa kwenye gari la shule kwenye eneo la bonde la Swat wiki hii. Malala ni mwanaharakati anayepigania haki ya kupata elimu jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa kundi la Taliban.

Madaktari wanaomtibu Malala wanasema kuwa hali yake kiafya inatoa matumaini kiasi ingawa ataendelea kubakia katika chumba cha wagonjwa mahututi. Wameweza kumtoa risasi kutoka katika bega lake. Serikali ya Pakistan imetangaza zawadi ya dola za Marekani 100,000 kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa watu waliofanya tukio hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: Getty Images

Taarifa zaidi zinasema kuwa familia ya binti huyo inasubiri muda wa masaa 48 upite ili kujua kama atapelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi au la. Baada ya masaa hayo madaktari ndio wataweza kutoa uamuzi juu ya kupelekwa nje ya nchi.

Shambulizi hilo limekemewa vikali na jumuiya ya kimataifa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani kitendo hicho. Rais Barack Obama wa Marekani pia amelaani tukio hilo akisema kuwa ni la kukera.

Mwandishi: Stumai George/AFP

Mhariri: Josephat Charo