1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya utumwa duniani

Volker Wagener / Maja Dreyer23 Agosti 2007

Utumwa unasemekana kuwa ni suala linalopitwa na wakati. Lakini ni kosa kubwa kuamini kuwa binadamu hatumiki tena kama bidhaa inayouzwa na kununuliwa. Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kumbukumbu za utumwa na kuangamizwa kwake, mwandishi wetu Volker Wagener anachunguza juu ya aina za utumwa wa kisasa ambazo ziko takriban duniani kote.

https://p.dw.com/p/CHjd
Nchini China watoto wanalazimisha kufanya kazi katika kiwanda cha matofali
Nchini China watoto wanalazimisha kufanya kazi katika kiwanda cha matofaliPicha: AP

Siku chache tu zilizopita habari kutoka Mauretania ilikuwa ya kushangaza: Bunge la nchi hiyo ya Afrika Magharibi limepitisha sheria ya kuweka adhabu kwa matumizi ya watumwa. Hata hivyo, utumwa umeshapigwa marufuku zaidi ya miaka 25 iliyopita. Kwa nani basi sheria hiyo inahitajika? Kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu, watu wa asili ya Kiafrika wanafanya kazi za kama watumwa katika nyumba za wakaazi wa asili ya Kiarabu.

Mfano mwingine ni China ambapo mamia na maelfu ya wanaume na watoto wanalazimika kufanya kazi ngumu katika viwanda vya kutengeneza matofali. Vilevile barani Amerika Kusini suala la utumwa bado halijakamilisha. Miezi miwili tu iliyopita polisi iliwakomboa wafanyakazi 1100 wa shamba ya miwa. Mwenyeshamba alitumia namna ya zamani kuwalazimisha watu hao kufanya kazi kwake: Kwanza aliwauzia maskini hao vitu kwa bei ya juu. Waliposhindwa kulipa basi aliwashurutisha kufanya kazi kwenye mashamba.

Mifano hiyo inaonyesha wazi kuwa utumwa bado uko katika ulimwengu wa sasa. Hasa ni aina fulani ya utumwa ambao unatumika katika maeneo mengi, yaani biashara ya watoto, kuwalazimisha watoto kufanya kazi ngumu na unyonyaji wa wafanyakazi. Mashirika mengi yanayotetea haki za binadamu yanachunguza hali ya wafanyakazi na kuona kesi nyingi za watu kunyonywa, hususan wanawake na wasichana wanaofanya kazi za nyumbani katika nyumba za wageni.

Bi Juliane Kippenberg wa shirika la Human Rights Watch, tawi la Ujerumani, alichunguza hali ya kazi ya wasichana nchini Guinea, Afrika Magharibi, naye anaeleza juu ya matokeo yake: "Tumeona kuwa kuna hali ya utumwa nchini Guinea kwa sababu wasichana wengi walilazimishwa kufanya kazi. Wengi wanafanya kazi ngumu, tena kwa muda wa saa 18 kila siku. Hawaruhusiwi kupumzika na hawapewi likizo. Juu ya hayo, wengi wao hawalipwi kwa kazi hiyo ngumu.”

Hali pia ni ngumu kwa wanawake katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kulingana na shirika na Umoja wa Mataifa, huko maelfu ya wanawake na wasichana wanaoishi katika eneo la vita hubakwa na kuuawa kwa namna mbaya sana. Katika mkoa wa Kivu Kaskazini pekee, kesi 5000 zimegunduliwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Kuhusiana na kazi za watoto, makampuni ya nguo barani Ulaya yanakosolewa vikali na mashirika ya haki za binadamu. Hivi punde tu ilifichuliwa kuwa mashati fulani ya kampuni ya “Esprit” yalikuwa yametengenezwa na watoto wenye umri wa miaka 11 nchini India ambao waliuzwa na wazazi wao kama watumwa.

Katika ujumbe wake maalum kwa siku ya leo, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mambo ya elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Bw. Koichira Matsuura alikumbusha pia juu ya utumwa katika wakati huu. Aidha ali taka kuhakikishwa kuwa watoto katika shule wanafundishwa historia juu ya biashara ya watumwa ili kutosahau sura hiyo mbaya na kuwafahamisha juu ya athari zake.