1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya vyombo vya habari duniani

3 Mei 2015

Leo(03.05.2015) ni Siku ya Vyombo vya Habari duniani: Kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Achia uwandishi habari ustawi! Kuelekea upashaji habari bora, usawa wa jinsia na usalama wa vyombo vya habari katika enzi ya dijitali.”

https://p.dw.com/p/1FJH9
Demonstration für die Freilassung französischer Journalisten
Maandamano yanayodai kuachiwa huru kwa waandishi habari wa Ufaransa AfghanistanPicha: picture alliance/dpa

Kila mwaka tarehe 3 Mei ni siku ambapo husherehekewa misingi ya vyombo vya habari, kutathmini hali ya vyombo vya habari duniani kote, kuvilinda dhidi ya mashambulizi kwa uhuru wao na kuwakumbuka waandishi habari waliopoteza maisha yao wakitekeleza majukumu yao.

Tag der Pressefreiheit 2009 Lateinamerika
Siku ya vyombo vya habari America ya kusiniPicha: picture alliance/dpa Fotografia

Tarehe 3 Mei ilitangazwa kuwa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari Duniani na Baraza kuu la Umoja wa mataifa mwaka 1993, kufuatia pendekezo lililopitishwa katika kikao cha mkutano mkuu wa Shirika la Elimu, sayansi na Utamaduni –UNESCO 1991.

Tarehe hii huwa ni wakati wa kuwaarifu raia kuhusu kukandamizwa kwa uhuru wa vyombo vya habari-kukumbusha kwamba katika nchi kadhaa duniani, maandishi na machapisho yanakaguliwa, wahusika kutozwa faini kuzuiwa kufanya kazi zao na hata kufungiwa-wakati waandishi habari, wahariri na wachapishaji wakiandamwa na kubughudhiwa, kushambuliwa, kukamata na kuweko vizuizini na hata kuuawa.

Kuba Bloggerin Yoani Sanchez Havana
Mwandishi wa Blog nchini Cuba Yoani SanchezPicha: picture alliance/dpa

Katika risala yake kuadhimisha siku hii, Mkurugenzi mkuu wa Unesco Irina Bukova alisema "Ili amani iweze kudumu, ili maendeleo yawe endelevu, wanawake na wanaume lazima wazungumze kwa uhuru, ili kujenga na kubadilishana maarifa na vyombo vya habari kila mahala. akaongeza , Uandishi habari wa uhakika huwaruhusu raia kufanya maamuzi juu ya maendeleo ya jamii zao kuchunguza masuala ya ukosefu wa haki, rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka."

Ripoti ya hivi karibuni ya taasisi inayojulikana kama Freedom House iliotolewa mjini Washington, imeeleza kwamba magaidi wanawalenga waandishi habari, serikali za kiimla zinawafunga na baadhi ya nchi zinaimarisha ukaguzi wa vyombo vya habari. Taasisi hiyo imesema hali ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ilididimia mwaka 2014, hadi kiwango kisichoshuhudiwa kwa zaidi ya miaka 10 iliopita.

Uhru wa habari wakandamizwa

Tathmini katika nchi na maeneo 199, imebainisha kwamba nchi ambako hali ya uhuru wa waandishi na vyombo vya habari kwa jumla ni mbaya zaidi ni Belarus, Crimea, Cuba, Guinea ya Ikweta, Eritrea,Iran na Korea kaskazini. Kwengineko ni Syria, Turkmenistan na Uzbekistan.

Bahrain Tag der Pressefreiheit Demonstration in Manama
Maandamano katika siku ya vyombo vya habari Bahran 2007Picha: AP

Tarehe 3 Mei ni siku ya kuzikumbusha serikali duniani juu ya haja ya kuheshimu ahadi zilizotolewa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha zinatekelezwa na pia ni siku ya kutafakari miongoni mwa wanahabari na vyombo vya habari kuhusu masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na maadili ya kiutendaji. Pia ni siku ya kuwakumbuka waandishi habari waliopoteza maisha yao wakiwa kazini au kwa kutetea walichokiamini kuwa ni uhuru wa kuuarifu umma.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman , UNESCO Website

Mhariri:Yusuf Saumu