1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sikulenga kumtusi Obama,Rais Duterte

Jane Nyingi6 Septemba 2016

Mkutano wa viongozi wa kusini mashariki mwa bara Asia kujadili ugaidi, usalama na mzozo wa eneo linalozozaniwa la bahari ya Kusini mwa China ulioanza Leo (06.09.2016) umepungua msisimko.

https://p.dw.com/p/1JwQl
Bildkombo Barack Obama und Rodrigo Duterte
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb/M. Dejeto

Hatua hiyo ni kutokana na matamshi machafu yaliyotolewa na rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, dhidi ya rais wa Marekani, Barack Obama.Tayari rais huyo amesema anajutia alichokisema baada ya kumuita Rais Obama "mwana wa kahaba".

Rais Duterte alimtupia cheche hizo za maneno mwenzake wa Marekani alipopewa nafasi ya kuzungumza wakati wa mkesha wa kikao cha ufunguzi wa mkutano huo unaowaleta pamoja viongozi wa mashariki na kusini mwa bara Asia. Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Duterte kuhudhuria mkutano huo unaofanyika kila mwaka baada ya kuchaguliwa urais mwezi Juni mwaka huu. "Mimi ni rais wa taifa huru na tulijikomboa zamani kutoka kwa mkoloni wetu. Hakuna mwingine anayepaswa kuniambia cha kufanya ila tu Wafilipino, hakuna, hakuna. Lazima uheshimu, sio kutupa tupa maneno na maswali " alisema Duterte.

Obama avunja mkutano na Duterte

Matamshi hayo yamempelekea Rais Obama kuvunja mkutano na rais huyo wa Ufilipino. Obama alisema alichotaka kumuuliza Rais Duterte ni kuhusu mauaji yanayoendelea nchini mwake dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika katika biashara ya madawa ya kulevya. Huu ungekuwa mkutano wake wa kwanza na Rais Duterte."Mimi kila mara nataka kuhakikisha iwapo natafanya mkutano, utakuwa wenye manufaa. Sisi tunatambua mzigo mzito unaosababishwa na biashara ya ulaguzi wa madawa ya kulevya sio tu Ufilipino bali pia ulimwengu mzima na kupiga vita biashara hivyo si jambo rahisi, lakini kila mara tunatetea kuhakikisha sheria inazingatiwa".

Laos ASEAN Gipfel Bounnhang Vorachith empfängt Barack Obama
Rais wa Marekani Barack Obama (Kulia) na mwenyeji wake Bounnhang Vorachith katika ikulu ya rais,Laos.Picha: Reuters/J. Silva

Msako dhidi ya walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya

Awali Rais Duterte alikuwa amesema hatakubali Rais Obama kumtolea mihadhara kuhusu haki za binadamu, na kuongeza kuwa watu wengine zaidi watauawa kabla ya kukamilika kamata kamata ya walanguzi na watumizi wa madawa ya kulevya, ambayo hadi sasa imeshasababisha vifo vya karibu watu 2,400 tangu rais huo kuingia madarakani miezi miwili iliyopita.

Philippinen festgenommene Drogendealer
Watumizi wa dawa za kulevya waliotiwa mbaroni kufuatia msako unaoendeshwa na serikaliPicha: Getty Images/D. Tawatao

Rais Obama sasa atakutana na atakutana na rais wa Korea kusini.Katika kikao cha leo, Rais Obama ameahidi kuwa Marekani itajitahidi kuondoa mamilioni ya mabomu yaliyoangushwa kisiri na ndege za Marekani miongo mingi iliyopita nchini Laos. Mashambulizi hayo yalifanyika kati ya mwaka 1964 na mwaka 1973 wakati Washington alianzisha vita vya siri vilivyooongozwa na Shirika lake la Kijasusi, CIA, kupunguza vifaa vilivyokuwa vikisafirishwa kwa wapiganaji wa kikomunisti wakati wa vita vya Vietnam. Nchi hiyo itapokea dola millioni 90 katika muda wa miaka mitatu kutoka Marekani kushughulikia athari zilizotokana na mabomu hayo.

Mwandishi: Jane Nyingi/AP/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef