1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha ndogo ndogo bado ni tatizo kubwa duniani

Saumu Mwasimba12 Agosti 2008

Jumuiya ya kimataifa kukutana Norway kujadiliana zaidi

https://p.dw.com/p/EvjK

Jumuiya ya kimataifa iliyojadiliana kwa mafanikio mikataba inayopiga marufuku matumizi ya mabomu ya kutegwa chini ya ardhi na mabomu yanayotawanyika-"cluster bomb", imepiga hatua ndogo mno katika kuandaa mkataba wa umoja wa mataifa kudhibiti kuenea kwa silaha ndogo ndogo. Hayo ni kwa mujibu wa umoja wa mataifa.

Licha ya uwezekano wa kupatikana jumla ya silaha ndogo ndogo 600 milioni katika masoko wazi na ya chini kwa chini, hakuna bado mkataba wa kimataifa wa kudhibiti kusambaa kwa silaha hizo.

Mtaalamu Natale J.Goldring kutoka taasisi ya taaluma ya masuala ya amani na usalama katika shule ya mambo ya nchi za nje ya Edmund.A.Walsh ambayo ni tawi la chuo kikuu cha Georgetown, serikali zina chaguo wazi nalo ni ama ziendelee na shughuli kama kawaida ambapo hali husababisha vifo vya watu karibu 1.000 kila siku kwa sababu ya matumizi ya silaha, au kufikia makubaliano yanayolazimishwa kisheria katika utekelezaji wake kuzuwia biashara ya silaha ndogo ndogo.

Umoja wa mataifa unadai kwamba, silaha ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na bunduki, silaha za kufyatulia maguruneti, bastola na bunduki za rashasha, ndizo zinazoonekana kutumika katika matukio ya aina hiyo na kuwa chanzo cha mauaji na uharibifu katika maeneo ya mizozo duniani.

Baada ya majadiliano, mkataba wa kimataifa ulisaini Canada mwezi Desemba 1997, kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini, wakati mkataba mpya unaopiga marufuku mabomu yanayotawanyika baada ya kuripuka utakua tayari kusainiwa nchini Norway mapema mwezi Desemba mwaka huu.

Judy Isacoff wa kituo cha Afrika cha taaluma ya masuala ya mkakati barani chenye makao makuu mjini Washington, anasema utapakazaji wa silaha ndogo ndogo linabakia kuwa moja wapo ya changa moto kubwa kuhusiana na usalama katika kanda ya maziwa makuu na ile ya Afrika mashariki.

Kituo hicho kitakua na warsha kuanzia tarehe 17 hadi 22 mwezi huu wa Agosti, kuchunguza sababu zinachangia kuzagaa kwa silaha ndogo ndogo na kuweka mikakati ya kupunguza wimbi hilo pamoja na kiu cha kutaka kuwa na silaha hizo.

Akihutubia mkutano kuhusu silaha ndogo ndogo mwezi uliopita, Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon alisema mataifa wanachama yamepiga hatua kubwa katika kupambana na silaha ndogo ndogo lakini bado kuna changamoto nyingi .

Mkurugenzi wa mtandao mmoja wa kimataifa unaopigania kuchukuliwa hatua madhubuti za kivitendo International Action Network Rebecca Peters,

anatoa mfano kwamba wakati wanachama wa umoja wa mataifa walipokua wakijadiliana kwa siku tano mwezi uliopita juu ya suala hilo, kaisi ya watu 5000 walikuwa wamepigwa risasi katika sehemu tafauti duniani.

Hali hii anasisisiza, inatoa changa moto kubwa juu ya haja ya kukabiliana na tatizo hili na kwamba linaweza tu kushughulikiwa vilivyo kwa ushirikiano wa pamoja kwa kuwa na muungozo wa pamoja kwa mataifa duniani.

Wakati walimwengu wakisubiri kukutana nchini Norway mwezi Desemba kwa hivyo ni muhimu kutambua kwamba umilikaji wa silaha ndogo ndogo kinyume cha sheria ni tatizo la dunia.