1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Simone Gbagbo jela miaka 20

Mohammed Khelef10 Machi 2015

Mahakama nchini Cote d'Ivoire imemuhukumu mke wa rais wa zamani, Simone Gbagbo, kifungo cha miaka 20 kwa kuuhujumu usalama wa nchi wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi kati ya mwaka 2010 na 2011.

https://p.dw.com/p/1Enwy
Simone Gbagbo, mke wa aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo.
Simone Gbagbo, mke wa aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo.Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Blackwell

Rais wa mahakama kuu, Tahirou Dembele, alisema hivi leo (tarehe 10 Machi) kuwa kwa kauli moja majaji waliosikiliza kesi hiyo waliipitisha adhabu hiyo dhidi ya Simone mwenye umri wa miaka 65, ambaye alionekana kwenye chumba cha mahakama akiwa na uso wa fadhaa, wakati hukumu dhidi yake ikisomwa.

Mke huyo wa rais wa zamani alitiwa hatiani pia kwa kuchafua amani na utulivu na kuandaa makundi yenye silaha, baada ya mumewe na wafuasi wake kuyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Disemba 2010 yaliyompa ushindi hasimu wake, Alassane Ouattara.

Wakili wake, Me Rodrigue Dadje, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mteja wake "hakushitushwa na adhabu hiyo" akisema kuwa wataikatia rufaa.

Baada ya hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Soungalo Coulibaly alisema wamefanikiwa kuionesha dunia kuwa tabia ya kutenda makosa na kisha mtu akakwepa mkono wa sheria haipaswi kuendelea nchini Cote d'Ivoire.

"Simone Gbagbo alishiriki kwa uhakika kabisa kwenye uundaji wa makundi yenye silaha, watu wake walishiriki kwenye vuguvugu la mauaji." Wakili wa serikali, Simon Yabo Obi, aliiambia mahakama hivi leo.

Enzi za kuwa madarakani, Laurent na Simone Gbagbo.
Enzi za kuwa madarakani, Laurent na Simone Gbagbo.Picha: Reuters/L. Gnago

Mtoto wa Gbagbo ahukumiwa miaka 5

Mtoto wa kiume wa Laurent Gbagbo aitwaye Michel, ambaye pia ana uraia wa Ufaransa, naye pia alihukumia kifungo cha miaka mitano jela kutokana na dhima yake kwenye ghasia hizo za baada ya uchaguzi.

Simone aliyekuwa akifahamika pia kwa jina la "Iron Lady", alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwezi Januari akiwa na wenzake 82 wakituhumiwa kuhusika na machafuko hayo katika viwango tafauti.

Suala muhimu kwenye kesi yake ilikuwa ni kuchunguza endapo alishiriki kwenye kuongoza vikosi vya mauaji ambayo yaliendelea kwa wiki kadhaa baada ya uchaguzi uliozozaniwa mwishoni mwa mwaka 2010. Waendesha mashitaka walikuwa wameomba adhabu ndogo ya kifungo cha miaka 10 jela.

Simone ajitetea

Hapo jana, mwenyewe Simone Gbagbo alitoa ushahidi wake kwa takribani masaa manne, akiwapinga vikali mashahidi waliosema walimuona akigawa silaha kwa vijana mjini Abdijan. Aliiambia mahakama hiyo kuwa anawasamehe wanaomtuhumu.

Simone Gbagbo akiongozwa na polisi kuingia mahakamani mjini Abdijan.
Simone Gbagbo akiongozwa na polisi kuingia mahakamani mjini Abdijan.Picha: picture-alliance/dpa/Koula

"Nimedhalilishwa ukomo wa kudhalilishwa kwenye kesi hii. Lakini niko tayari kusamehe kwa sababu ikiwa hatusamehe, nchi hii inakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi kuliko tulioushuhudia," alisema Simone mahakamani hapo, akisisitiza kuwa hajioni na hatia yoyote na kwamba mumewe, Laurent Gbagbo, alishinda kihalali uchaguzi wa 2010.

Takribani watu 3,000 walipoteza maisha yao kwenye ghasia za miezi kadhaa baada ya uchaguzi huo, ambazo zilizimwa na uingiliaji kati wa wanajeshi wa kimataifa chini ya idhini ya Umoja wa Mataifa wakiongozwa na mkoloni wa zamani, Ufaransa.

Laurent Gbagbo mwenyewe yuko kizuizini katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, Uholanzi, anakokabiliwa na kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou