1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIPRI: Matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani

Amina Mjahid
22 Aprili 2024

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani na usalama SIPRI, imesema matumizi ya kijeshi kote duniani yameongezeka kwa asilimia 7, ikiwa ni sawa na dola trilioni 2.43 kwa mwaka 2023

https://p.dw.com/p/4f2fz
Matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani kote
SIPRI yasema nchi kumi zilizokuwa na matumizi makubwa ya kijeshi kwa mwaka 2023 zimeongozwa na Marekani, China na Urusi. Picha: Wojtek RADWANSKI/AFP

Taasisi hiyo ya SIPRI iliyoko mjini Stockholm, Sweden, imesema ongezeko hilo la asilimia 7 ni kubwa tangu mwaka 2009 huku ikiongeza kwamba nchi kumi zilizokuwa na matumizi makubwa ya kijeshi kwa mwaka 2023 zimeongozwa na Marekani, China na Urusi.

Nan Tian, Mtafiti Mkuu katika mpango wa uangalizi wa matumizi ya kijeshi na utengenezaji wa silaha wa SIPRI, amesema ongezako linaloonekana limetokana na kudorora kwa amani na usalama wa dunia.

Tian amesema mataifa yanaweka mbele nguvu za kijeshi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama wa dunia. SIPRI imesema Urusi kwa mfano, imeongeza matumizi yake kwa asilimia 24 ambayo ni sawa na dola bilioni 109. Ukraine nayo imeongeza matumizi hayo ya kijeshi kwa asilimia 51, sawa na dola bilioni 65 na kupokea angalau dola bilioni 35 za msaada wa kijeshi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi.

Mauzo ya silaha Ulaya yaongezeka kwa vita vya Ukraine

SIPRI imeongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO zimetumia takriban asilimia 55 ya matumizi ya kijeshi duniani. Mtafiti mwengine wa SIPRI, Lorenzo Scarazzato, amesema miaka miwili ya vita vya Urusi nchini Ukraine imebadilisha kabisa muonekano wa usalama na kutoa kitisho zaidi cha usalama badala ya amani na uthabiti duniani.

DR Kongo ni miongoni mwa nchi zilizokuwa na matumizi makubwa mno ya kijeshi

Kundi la waasi wa M23
Waasi wa M23 waliosambaratisha usalama wa Mashariki mwa Kongo Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/File/picture alliance

Katika Mataifa ya Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliongeza matumizi yake kwa asilimia 105, ikiwa moja ya nchi iliyo na matumizi makubwa mno ya kijeshi, mwaka 2023 na watafiti wanasema ongezeko hili bila shaka limetokana na mgogoro unaoendelea kati ya serikali, na makundi yaliojihami ya waasi.

Migogoro ya kikanda na uboreshaji wa kijeshi pia ni miongoni mwa mambo yaliyoongeza matumizi ya kijeshi, kwa mfano mgogoro kati ya China na Taiwan umetajwa katika ripoti hiyo kama moja ya vita vilivyoongeza matumizi ya kijeshi ya mataifa maeneo hayo mawili. China, iliongeza matumizi yake kwa asilimia 6 nazo Japan na Taiwan zikaongeza matumizi yao kwa asilimia 11.

SIPRI: Mapato ya makampuni makubwa ya silaha yapungua

Watafiti wa taasisi hiyo wamesema wanakadiria katika utafiti watakaoufanya wa mwaka 2024 matumizi ya kijeshi huenda yakaongezeka zaidi kufuatia shambulizi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas, katika Ukanda wa Gaza na wasiwasi uliopo katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati ya mzozo kutanuka pia, umesababisha matumizi hayo kuongeza kwa kiasi kikubwa kuwahi kushuhudiwa ndani ya miaka 10 iliyopita.

reuters /dpa/ DW