1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Snowden aomba hifadhi ya muda Urusi

13 Julai 2013

Mfichua siri za Marekani Edward Snowden amesema anatafuta hifadhi ya muda nchini Urusi hadi pale atakapoweza kuenda Amerika ya kusini ambako nchi kadhaa zimeashiria kuwa tayari kumpa hifadhi

https://p.dw.com/p/1979y
Picha: Reuters

Katika mkutano wake wa kwanza tangu akimbilie Urusi kutoka Hong Kong na kukwama katika uwanja wa ndege wa Moscow kwa wiki tatu sasa,Snowden hapo jana(12.07.2013) alikutana na wanaharakati wa Urusi na mawakili.

Bado anatafuta mahali salama ili kukwepa kushitakiwa na Marekani kwa makosa ya kufichua siri za serikali kuhusiana na mpango wake wa kuyapeleleza mawasiliano ya simu ya na ya kwenye mtandao.

Snowden na wanaharakati wa Urusi
Snowden na wanaharakati wa UrusiPicha: Reuters

Hata hivyo Marekani imezidisha shinikizo kwa Urusi kwa kuionya nchi hiyo dhidi ya kumruhusu Snowden kuendelea kuwepo nchini humo na kuendelea kuifedhehesha Marekani kwa kufichua siri zaidi.

Snowden aweka uhusiano wa Urusi na Marekani matatani

Wakati huo huo Rais wa Marekani Barrack Obama amezungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa njia ya simu baada ya Marekani kuionya Urusi kutompa afisa huyo wa zamani wa kijasusi jukwaa la kueneza propaganda.

Maafisa waandamizi wa Marekani wameonya kuwa kumpa Snowden hifadhi itakuwa ni kukingamana na msimamo wao wa awali kuwa Urusi haitataka kuuzorotesha uhusiano wake na Marekani kutokana na kashfa hiyo na kuahidi kutoegemea upande wowote.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney ameitaka Urusi imfukuze Snowden ili arejeshwe Marekani kujibu mashitaka kwa kufichua siri za usalama wa kitaifa.

Rais wa Nicaragua Daniel Ortega na wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Nicaragua Daniel Ortega na wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture-alliance/dpa

Snowden alionekana hapo jana kwa mara ya kwanza tangu alipowasili katika uwanja wa ndege wa Moscow akiwa na wawakilishi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights watch na Amnesty International.

Snowden mwenye umri wa miaka 30 alisema amepokea uungwaji mkono na hifadhi ambazo amepata kufikia sasa na kwamba uamuzi wake kuuambia ulimwengu kuhusu mipango ya udukuzi ya nchi yake imemgharimu lakini ndilo jambo jema la kufanya na hajuti kufanya hivyo.

Mfichua siri huyo ambaye hana hati za kusafiria amesema anatumai Urusi itakubali ombi lake la hifadhi ya muda ili aweze kupanga jinsi ya kusafiri kwa kufuata sheria hadi Amerika ya kusini.

Amerika ya kusini yaridhia hifadhi

Licha ya nchi nyingi ambazo alikuwa ametuma maombi ya hifadhi kuyakataa maombi yake,Venezuela,Bolivia na Nicaragua zimeridhia kumpa hifadhi.

Viongozi wa Amerika kusini wametetea uamuzi wao wa kumpa hifadhi katika mkutano wa kanda hiyo unaofanyika nchini Argentina.

Mkutano huo pia umelaani kisa cha mapema mwezi huu ambacho nchi kadhaa za Ulaya zilikataa ndege iliyokuwa imembeba Rais wa Bolivia kutumia anga zake na kuilazimisha kutua Vienna nchini Austria kutokana na tuhuma kuwa Snowden alikuwamo ndani ya ndege hiyo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Mtullya Abdu.