1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Snowden na mifuko ya plastiki magazetini

4 Novemba 2013

Kama mfichua siri wa kimarekani apatiwe kinga ya ukimbizi Ujerumani na namna ya kuepukana na mzigo wa mifuko ya plastiki barani Ulaya ndizo mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1AB9i
Waandamanaji wanaomuunga mkono Edward Snowden wamekusanyika mbele ya jengo la bunge la shirikisho-Bundestag mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini na kashfa ya upelelezi uliofanywa na idara ya ujasusi ya Marekani-NSA dhidi ya raia mpaka viongozi wa taifa na serikali katika pembe tofauti za dunia.Mfichua siri zote hizo ni Edward Snowden ambae hivi sasa amekimbilia Urusi.Sauti zinasikika kudai kijana huyo akubaliwe hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.Gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linaandika":Pengine kutokana na hali namna ilivyo hivi sasa serikali ya mjini Berlin inaweza kujitetea mbele ya Washington na inaweza pengine hata kusimama kidete kupinga,kwa muda mfichua siri huyo pindi akifika katika ardhi ya Ujerumani,asirejeshwe Marekani.Lakini baadae je?Milele Ujerumani haitoweza kufanya hivyo.Miaka miwili,mitatu au pengine hata minne,uhusiano kati ya Berlin na Washington utarejea kuwa wa kawaida.Lakini Washington kamwe haitamsahau Snowden.Na hakuna nchi yeyote ambako Snowden atakuwepo,itakayoweza kutegemea hisani ya Marekani.

Gazeti la mjini Oldenburg "Nordwest Zeitung "linajiuluza kwanini Edward Snowden amekubaliwa hifadhi ya ukimbizi nchini Urusi.Gazeti linaendelea kuandika:" Kusema kweli uamuzi wa ikulu ya Urusi umechochewa na mbinu za kuonyesha misuli ya kiasiasa.Kila wakati ambapo Snowden atakapozidi kufichua siri za idara za upelelezi za Marekani dhidi ya viongozi wa serikali ya Ujerumani na wa serikali nyengine za Ulaya,ndipo nazo lawama dhidi ya Washington zitakapozidi kutolewa mjini Berlin,Paris ,Madrid na kwengineko.Putin anaweza kulijongelea zaidi bara la Ulaya.Ndio maana serikali kuu ya Ujerumani inabidi izingatie:Ufafanuzi,sawa lakini isisahauliwe kwamba wamarekani ni washirika wetu."

Edward Snowden Ehrenurkunde Whistleblower-Preis 2013 BILDAUSSCHNITT
Edward Snowden akionyesha shahada ya tuzo ya mfichua siri ya mwaka 2013 aliyokabidhiwa na Hans-Christian Ströbele wa chama cha walinzi wa mazingira cha UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Sifa ya Marekani haichujuki

Maoni sawa na hayo yametolewa pia na gazeti la "Münchner Merkur" linaloandika:"Baada ya kufichua harakati za upelelezi za Marekani,watu hawawezi kusahau mara moja kilichotokea.Na Edward Snowden aliyefichua vifa hivyo vya uhalifu,hastahiki kutokomea katika jela za Marekani.Inahitajika ridhaa kutoka kila upande hadi kufikia uwezekano wa kusamehewa Snowden na taasisi za sheria za Marekani.Ingawa ghadhabu zilizosababishwa na kusikilizwa mawasiliano ya simu za mkononi za kansela ni za haki hata hivyo watu wasisahau kashfa ya NSA haitoichafua hata kidogo sifa ya kihistoria ya Marekani katika kuleta amani,uhuru na neema nchini Ujerumani.

Plastiktüten auf wilder Müllhalde
Mifuko ya plastiki imeenea majiani:picha hii imepigwa Pakistan februari 25 mwaka huu wa 2013Picha: CC/Zainub Razvi

Dawa ya miifuko ya plastiki

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mikoba ya plastiki na namna ya kupambana na mikoba hiyo inayozidi kuchafua mazingira.Gazeti la "Nordbayerischer Kurier"linaandika: "Hakiingiii mfukoni"-wachache ndio wanaosema hivyo.Mashirika ya usafi wa mazingira yanakadiria pekee nchini Ujerumani mifuko elfu kumi inatumika kila dakika moja!Asili mia 95 ya ndege waliofariki katika fukwe za bahari ya kaskazini,wamegunduliwa na vipande visivyopungua 30 vya mifuko hiyo ya plastiki mwilini mwao.Binaadam unaposikia habari hizo unashtuka kwanza lakini unapokwenda dukani,unaununua tena mfuko huo.Kwa hivyo bora mfuko wa plastiki uwe ghali kwanamna ambayo hakuna ataekusubutu tena kuutupa ovyo ovyo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu