1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia na mkutano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Afrika

Oumilkheir Hamidou
10 Februari 2017

Uchaguzi wa rais Somalia, mkutano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na nchi za Afrika mjini Nairobi na jinsi nchi za Ulaya zinavyopanga kujikinga dhidi ya wahamiaji ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii.

https://p.dw.com/p/2XKB7
Kenia Nairobi Amina Mohamed und Brigitte Zypries
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim

Tunaanzia lakini moja kwa moja Mogadishu ambako zoezi la aina yake la kumchagua rais lilikamilika wiki hii kwa kuchaguliwa waziri mkuu wa zamani Mohammed Abdullahi Mohammed, maarufu kwa jina "Farmajo kuwa rais mpya wa Somalia. "Somalia rais huchaguliwa na bunge ambalo lenyewe huchaguliwa na wachache" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Munich, "Süddeutsche".

Gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani linazungumzia jinsi mabango yenye picha za wagombea yalivyoenezwa katika barabara za mji mkuu Mogadishu, kila mmoja akitoa ahadi zake - na kwa pamoja wakiahidi "hali itakuwa bora". "Kwani wananchi wana chaguo jengine"? linajiuliza gazeti la Süddeutsche linalowanukuu viongozi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wakiutaja uchaguzi huo wa aina yake kuwa ni "hatua muhimu baada ya miongo kadhaa ya vurugu."

Kila mdau anapigania masilahi yake Somalia

Ingawa Somalia inatajwa kuwa nchi mojawapo miongoni mwa nchi maskini kabisa ulimwenguni, hata hivyo ni nchi inayowashughulisha wadau wengi pia wa dunia, linaandika Süddeutsche linalozitaja Athiopia, Qatar, Sudan, nchi za ulaya na Marekani na wengineo kuwa miongoni mwa wadau hao. Kati yao kuna wanaomtaka mgombea wa kabila hili au lile na wengine wanaopigania ifuatwe itikadi kali ya kidini au wangineo wenye masilahi yao katika sekta ya mafuta, linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche.

 Mkutano wa akiuchumi kati ya Ujerumani na Afrika mjini Nairobi

Wanauchumi wa Ujerumani wavutiwa na bara la Afrika, ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Düssedoorf, Handelsblatt linaloshughulikia masuala ya biashara. Gazeti linazungumzia kuhusu mkutano wa kiuchumi ulioitishwa wiki hii mjini Nairobi Kenya kati ya Ujerumani na mataifa ya Afrika. Makampuni ya Ujerumani yamepania kutoiachia China peke yake uwanja barani Afrika , yanasaka njia za uwekezaji katika bara hilo jirani. Kufuatia mkutano huo wa siku mbili uliohudhuriwa na wawakilishi 500, takriban nusu wakitokea Ujerumani, Handelsblatt linahisi serikali kuu ya Ujerumani imeshaanza kuona tija ya mipango  yake kwa Afrika.

Mawaziri wa uchumi Brigitte Zypries na mwenzake wa misaada ya maendeleo Gerd Müller walihudhuria mkutano huo uliofunguliwa kwa pamoja na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Makampuni mengi ya Ujerumani yanaashiria kuongezeka bei za mali ghali kutasaidia kuinua  uchumi katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara linaloitwa hivi sasa "Bara la Matumaini."Handelsblatt limekumbusha biashara ya Ujerumani kwa mataifa 49 ya kusini mwa jangwa la Sahara ilifikia Euro bilioni 26, kiwango ambacho ni sawa na kile cha biashara kati ya Ujerumani na Slovakia.

 Afrika Kipaumbele katika zamu ya Ujerumani kama mwenyekiti wa G-20

Mkutano mkuu wa kiuchumi kati ya Ujerumani na nchi za Afrika umeripotiwa pia na gatezi la Frankfurter Allgemeine linalojiuliza kama Ujerumani inaweza kusaidia kuinua uchumi barani Afrika. Gazeti hilo linamulika zaidi azma ya waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller ya kuanzisha mpango wa kuhimiza nidhamu na maendeleo , mpango unaolinganishwa na ule wa Marekani kwa Ujerumani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia-Marshal Plan. Frankfurter Allgemeine limekumbusha Ujerumani ndio mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya mataifa 20 muhimu kiuchumi-G-20 na kwamba serikali kuu imelitanguliza mbele bara la Afrika katika ajenda yake.

Ulaya yajijeengea kuta kujikinga dhidi ya wahamiaji kinyume na sheria

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inamulika mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa 32 ya Ulaya na Umoja wa Ulaya  na wenzao 34 wa Afrika ulioitishwa mjini Valletta kisiwani Malta. Mada kuu ni kutathmini namna ya kuzuwia wimbi la wahamiaji wanaoyatia hatarini maisha yao kwa lengo la kuingia Ulaya kupitia bahari ya kati.

Ulaya inajijengea ukuta, ndio kichwa cha maneno cha die Tageszeitung linalozungumzia jinsi misimamo ya pande hizo mbili zinavyotofautiana katika suala la wahamiaji. Gazeti limemnukuu mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya bibi Federica Mogherini akisema suala la uhamiaji linaweza kusiammiwa tu kupitia ushirikiano wa dhati.

 

Mandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo