1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yapinga makubaliano ya Ethiopia-Somaliland

Grace Kabogo
2 Januari 2024

Baraza la Mawaziri la Somalia limeutangaza mkataba uliofikiwa kati ya jimbo lake lenye utawala wa ndani, Somaliland, na taifa jirani la Ethiopia, hauna uhalali na haufai.

https://p.dw.com/p/4anIB
Mji wa bandari wa Berbera Somalia
Berbera ni mji wa bandari kaskazini mwa Somalia kwenye Ghuba ya Aden, katika jimbo la Somaliland lisilotambulika kimataifa.Picha: Yannick Tylle/picture alliance

Kikao cha Baraza la Mawaziri la Somalia kilichoongozwa na Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre kimefikia uamuzi huo huku waziri mkuu huyo akisema serikali yake itatumia kila njia ya amani iliyonayo kulinda mipaka na mamlaka yake.

Bofya hapa kusoma habari hii: Somalia kujadili makubaliano ya Somaliland na Ethiopia

Ofisi ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud bado haijazungumza chochote kuhusu hatua hiyo. Lakini rais wa zamani wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa makubaliano hayo yanasababisha wasiwasi mkubwa kwa Somalia na Afrika kwa ujumla.

Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Reuters/T. Negeri

Awali msemaji wa serikali ya Somalia anayeshughulikia masuala ya Somaliland, Abdikarim Hussein Guled alikuwa amesema serikali ya mjini Mogadishu, itajibu hatua hiyo kwa kutoa kauli kali na thabiti.

Hussein aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa vitendo vya serikali ya Ethiopia vinajumuisha kupuuza kwa wazi kanuni na mifumo ya sheria ya kimataifa, inayowakilisha ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya eneo la Somalia na kudhoofisha maendeleo yaliyopatikana kupitia mazungumzo yanayoendelea kati ya FGS, yaani Serikali ya Shirikisho ya Somalia na Somaliland ambayo yalikuwa yanakaribia kufikia azimio.

Makubaliano ya Somaliland na Ethiopia yalisainiwa jana Jumatatu mjini Addis Ababa, kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Somaliland, Muse Bihi Abdi, ambaye alisema haya baada ya kuyasaini:

''Tuna furaha sana, na tunamshukuru waziri mkuu wa Ethiopia tunaposaini mkataba huu. Tunawaruhusu watumie kilomita 20 za Bahari yetu na pia watatutambua kama nchi huru. Watakuwa taifa la kwanza kuitambua Somaliland baada ya kusainiwa kwa mkataba huu wa maelewano."

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Picha: Feisal Omar/REUTERS

Ethiopia, nchi ambayo haina eneo linalounganishwa na bahari, wala bandari, inategemea zaidi nchi jirani ya Djibouti katika biashara yake ya baharini.

Aidha, makubaliano hayo yamesainiwa siku chache tu baada ya serikali kuu ya Somalia na Somaliland kukubaliana kuanza tena mazungumzo ya kutatua mizozo yao, kutokana na juhudi za upatanishi zilizofanywa na Djibouti.

Fahamu kuhusu: Utawala wa Somaliland umesema hauna mpango wa kujiunga tena na Somalia

Mshauri wa usalama wa taifa wa Ethiopia, Redwan Hussein amesema makubaliano hayo ya kimataifa yanafungua njia kwa Ethiopia kuendesha shughuli zake za baharini kwenye eneo hilo, na kuiwezesha kuifikia kambi ya jeshi iliyokodishwa katika Bahari ya Shamu, njia kuu ya biashara ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Redwan, kwa upande wake, Somaliland itapokea sehemu ya mapato ya Shirika la Ndege la Ethiopia. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu hilo.