1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Southgate kumaliza kipindi cha mpito

Sekione Kitojo
14 Novemba 2016

Kocha wa mpito wa Uingereza  Gareth Southgate anakabiliana  na  mtu  anayetaka  kumuiga  katika  uchezaji wa  timu  na  hadhi  katika mchezo  wa  kesho  wa  kirafiki dhidi  ya Julen Lopetegui  wa Uhispania.

https://p.dw.com/p/2SgSo
Fußball England v Schottland - FIFA 2018 World Cup Qualifier
Wayne Rooney akishangiria bao na Adam Lalana dhidi ya ScotlandPicha: Getty Images/S. Botterill

Mchezo  huo  katika  uwanja  wa  Wembley  utakuwa  wa nne  na  wa   mwisho  kwa  kipindi  cha  mpito  cha Southgate  na  kufuatia  ushindi  wa  mabao  3-0  siku  ya Ijumaa  dhidi  ya Scotland   katika  mchezo  wa  kuwania kufuzu  kucheza  fainali  za  kombe  la  dunia , anatarajiwa kukabidhiwa  jukumu  kamili  la  kuifunza  timu  hiyo  ya taifa  ya  England.

Kama  alivyo  Southgate , Lopetegui  amepata  kuaminika na  chama  cha  kandanda  nchini  Uhispania  kwa  kuwa kocha  bora  katika  timu  ya  vijana  chini  ya  miaka  21, wakati  mchezo  wa  kujiamini  wa  kupasiana  mpira  wa Uhispania  ni  kitu  ambacho  Southgate  anataka  England iufuate.

Gareth Southgate
Kocha wa mpito wa Uingereza Gareth SouthgatePicha: Imago/Eibner Europa

Kocha  wa  Marekani  Jergen Klinsmann  ameitaka  timu yake  kukusanya  hisia  za  hasira  wakati  wanajaribu kurejea  katika  hali  ya  kawaida  kutoka  katika  kipigo dhidi  ya  Mexico  katika  mchezo  wa  kuwania  kufuzu kucheza  katika  fainali  za  kombe  la  dunia  dhidi  ya Costa  Rica  kesho  Jumane (15.11.2016).

Kikosi  cha  kocha  Klinsmann  kilipata  pigo  kubwa  dhidi ya  Mexico  siku  ya  Ijumaa, wakati Rafa Marquez alipofunga  katika  dakika  ya  89  bao  muhimu  katika ushindi  wa  mabao  2-1  katika  uwanja  wa  Mapfre.

Kipigo  hicho  kilikuwa  ni janga  kubwa  kwa  Marekani katika  duru  ya  ufunguzi  wa  mchezo  wa  kufuzu kucheza  katika  fainali  za  kombe  la  dunia  mwaka  2018 nchini  Urusi   katika  kanda  ya  CONCACAF.

Wakati  kumebakia  pointi  nyingi  za  kuwania  katika  duru ya  timu sita, Marekani  inahaha  kuzuwia  kupoteza michezo  zaidi  na   kukimbiwa  na  Mexico  na  Costa  Rica , mahasimu  wao  wakubwa  katika  kupata   nafasi  za moja  kwa  moja  za  kufuzu  kucheza  fainali  za  kombe  la dunia.

USA FIFA World Cup 2018 Qualifikation USA vs Mexiko
Kocha wa Marekani Juergen KlinsmannPicha: Reuters/USA Today Sports/T. Ruszkowski

Timu  tatu  zitakazomaliza  juu  ya  msimamo  wa  kundi hilo, zinafuzu  moja  kwa  moja  kuingia  katika  fainali  za dunia  wakati  timu  ya  nne  inaingia  katika  mchezo  wa mchujo.

Na  huko  mashariki  ya  mbali, kocha  Marcello  Lipi amesema  China  inahitaji  kuondokana  na  fikira  za  kuwa wanyonge  wakati  watakapopambana   katika  mchezo mgumu  wa  kwanza  akiwa  kama  kocha  wa  timu  hiyo, mchezo  wa  kufuzu  kucheza  katika  fainali  za  kombe  la dunia  dhidi  ya Qatar, mchezo  ambao  kila  timu haithubutu  kushindwa.

Wakati  Lippi , ambaye  aliifunza  Italia  na  kushinda kombe  la  dunia  mwaka  2006, anakiri  kwamba  China iliyoko  chini  kabisa  ya  msimamo  wa  kundi  la  mataifa ya  kanda  hiyo  inahitaji  maajabu  iwapo  inataka   kufika katika  fainali  za  kombe  la  dunia  mwaka  2018, amesema  umihimu  kwake  ni  kurejesha  imani.

"Ni  muhimu  kurejesha  imani  ya  timu," amesema  Lippi , kwa  mujibu  wa  tovuti  ya  FIFA, kabla  ya  pambano  la kesho Jumanne mjini  Kunming.

 

Mhariri: Yusuf  Samu