1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Soyinka achana kibali cha kuishi Marekani

Mohammed Khelef
2 Desemba 2016

Mshindi wa nishani ya fasihi ya Nobel kutoka Nigeria, Wole Soyinka, amerejesha kibali chake cha ukaazi nchini Marekani akilalamikia ushindi wa Donald Trump.

https://p.dw.com/p/2TciZ
Wole Soyinka
Picha: Andreas Rentz/Getty Images

Akizungumza na kituo cha habari cha eNCA na taarifa zake kunukuliwa na shirika la habari la Reuters, Soyinka mwenye umri wa miaka 82 amethibitisha kuwa ametekeleza kile alichoiita nadhiri yake ya kuhama Marekani, endapo Trump angeshinda urais wa taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa duniani.

Akizungumza akiwa mjini Johannesburg, Afrika Kusini, anakoshiriki kongamano la vyuo vikuu, mwandishi huyo mashuhuri wa fasihi alisema baada ya kumaliza taratibu zote za uhamaji, aliondoka Marekani.

Mkosoaji huyo mkubwa wa tawala za nchini kwake Nigeria, amekuwa akiishi Marekani tangu katikati ya miaka ya '90, akifundisha vyuo vikuu mbalimbali.

Ushindi wa Trump mwanzoni mwa mwezi uliopita, uliwashitua wengi, wakiwemo wasomi kama yeye, lakini Soyinka amekuwa mtu wa kwanza mashuhuri kuchukua hatua kama hii.