1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD wafuata mrengo wa kati

Hamidou, Oumilkher15 Septemba 2008

Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu chama cha Social Democratic chaamua kuelemea mrengo wa kati

https://p.dw.com/p/FIQF
Kiongozi mteule wa SPD Münterfering na mgombea wa kiti cha kansela SteinmeierPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamejishughulisha zaidi na matarajio ya chama cha Social Democratic -SPD,kansela wa zamani Helmut Schmidt anamlinganisha-japo si moja kwa moja- mkuu wa chama cha Die Linke,Oscar Lafontaine na Adolf Hitler na ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki,Benedikt wa 16 nchini Ufaransa.Tuanze lakini na mada ya mwanzo.Kiongozi mteule wa chama cha SPD-Franz-Münterfering amesema mwishoni mwa wiki,kuna uwezekano mzuri wa kuunda serikali ya muungano pamoja pia na chama cha kiliberali cha FDP.Gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG la mjini Gera linachambua:



"Hata kama vizingiti vya kuunda serikali kama hiyo ya muungano viko pale pale,lakini  viongozi wepya Franz Münterfering na Frank-Walter Steinemeier wanakipatia sura mpya SPD kwa kukinyemelea chama cha kiliberali cha FDP.Badala ya kila siku kugonga vichwa vya habari kwasababu ya kutaka kushirikiana na chama cha mrengo wa shoto Die Linke,hivi sasa SPD wanapalilia wenyewe mjadala badala ya kuchochewa na wengine.Hapo mtu anaona  tofauti iliyoko kati ya Kurt Beck na waliomfuatia."



Hata gazeti la OSNABRÜCKER ZEITUNG linaivulia kofia hatua ya viongozi wa SPD.Gazeti linaendelea kuandika:



"Badala ya kusalia kuwatumbulia macho  wafuasi wa mrengo wa shoto, Die Linke,wanaonyesha kuwavutia wale wasiopendezewa na ajenda 2010,SPD imeamua kujitambulisha upya na mkondo wa mageuzi.Mtindo wa kuunyemelea mrengo wa shoto waonyesha umekoma-angalao kwa sasa.Nacho chama cha Die Linke,kilichokua kikijipigia upatu kugeuka nguvu muhimu ya kisiasa,kitapwaya na kuendelea kuwa chama cha upinzani kisichokua na ushawishi wowote.SPD wameamua kufuata mrengo wa kati.Na huko ndiko wengi waliko na huko ndiko kwenye ufunguo wa kuingia madarakani."



Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linahisi ni sawa kama Steinmeier na Münterfering wataanza kujitafutia washirika wa serikali ya muungano.Gazeti linaendelea kuandika:


"Hawana chaguo jengine.Hawako tayari kushirikiana na mrengo wa shoto.Hali hiyo inamaanisha,SPD wakishindwa uchaguzi,basi wasocial Democratic hawatakawia kuelemea mrengo wa shoto chini ya uongozi wa Nahles na Wowereit.


Kuhusu  madai ya kansela wa zamani Helmut Schmidt kwamba Lafontaine anafanana na Adolf Hitler,gazeti la RHEINISCHE POST linaandika:


"Ni upuuzi mtupu aliosema Helmut Schmidt.Mbinu za kutaka kumzuwia Lafontaine kwa kumlinganisha na Hitler au hata Le Pen hazina maana.Badala yake zitapelekea kumpatia mshikamano ambao hajaustahiki.Lafontaine anapenda kucheza na maneno,hapimi-hata ya siasa kali za mrengo wa kulia ameshawahi kuyatumia.Anazungumzia juu ya "wafanyakazi wa kigeni" anachochea pia  chuki dhidi ya wanauchumi na dhidi ya Marekani.Watu wanaweza tuu kumzuwia kwa kubainisha asemeyo hayana ukweli"



 Na hatimae ni kuhusu ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16 nchini Ufaransa.Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaonyesha kustaajabishwa na umoja uliojitokeza kati ya jamhuri inayotenganisha siasa na dini na Vatikan.Gazeti linaendelea kuandika:



"Wasomi wa Ufaransa wanapozungumzia juu ya kanisa,hadi wakati huu wamekua wakishadidia juu ya "utaratibu wa kutojumuisha dini katika masuala ya kisiasa ya nchi yao.Rais Nicholas Sarkozy amekuja na neno jipya "utaratibu wa maana" akimaanisha uungaji mkono wa kanisa katika masuala ya kimoyo ya baadhi ya raia ambayo serikali haina jibu ,kuanzia katika shule hadi kufikia gerezani.Itakua wazimu,anasema Sarkozy,kujinyima imani za kidini.Hajasema hayo ili kumfurahisha Papa tuu,hasha,huo ndio ukweli unaojitokeza katika mji mkuu wa hikma barani Ulaya."