1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sri Lanka yatangaza kumalizika kwa vita.

18 Mei 2009

Serikali ya Sri Lanka imetangaza rasmi kuwa , kiongozi wa Tamil Tigers Velupillai Prabhakaran ameuawa.

https://p.dw.com/p/Hsa1
Raia watoroka mapigano kati ya wanajeshi wa Sri Lanka na Tamil Tigers.Picha: AP


Kifo cha Prabhakaran kimetokea saa chache baada ya mkuu wa majeshi nchini Sri Lanka kutangaza kumalizika kwa vita vya miaka 26, vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuwaangamiza wapiganaji wa Tamil Tigers.

Sri Lanka Tamil Tigers Rebellen
Tamil Tigers wameendeleza vita vya kujitenga tangu mwaka wa 1983.Picha: AP

Kuuawa kwa Prabhakan kunafunga ukurasa wa vita vya miongo mitatu vya wapiganaji wa Kitamil kutaka taifa lao huru. Wafuasi wake walimuabudu na kumstahi kama mkombozi- wapinzani wake walimtaja kama katili- ndivyo alivyotambulika Velupillai Prabhakan kiongozi wa kundi la Tamil Tigers aliyeongoza uasi dhidi ya serikali ya Sri Lanka tangu mwaka 1972.


Aliwekwa daraja moja na viongozi wengine walioongoza mapindunzi nchini mwao kama Ahmad Shah Masoud nchini Afghanistan na Che Guevarra huko Cuba. Lakini mwisho wake ulifikia mikononi mwa wanajeshi wa serikali. Karibu mwezi sasa serikali ya Sri Lanka iliamua kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa kitamil - na leo mkuu wa majeshi nchini Sri Lanka alitangaza kumalizika kwa vita hivi - vilivyoanza tangu mwaka wa 1983.


Sri Lanka Präsident Mahinda Rajapaksa
Mahinda Rajapaksa, rais wa Sri lanka aliapa kuwaaangamiza Tamil Tigers.Picha: AP

Jeshi la Sri lanka limesema limeyakomboa maeneo yote yaliyokuwa yanashikiliwa na Tamil Tigers- kwa miaka 26. Serikali ya Sri Lanka ilikatalia mbali mwito wa jumuiya ya kimataifa kusitisha vita ili kuwaokoa raia waliokuwa wanaathirika pakubwa. Msemaji wa wizara ya ulinzi Kaheliya Rambukwella alisema Sri Lanka iliamua safari hii itapambana na wapiganaji wa kitamil hadi mwisho.


Jumuiya ya ulaya imesema itaitisha uchunguzi ufanywe na hatua kuchukuliwa dhidi ya madai kwamba serikali ya Sri Lanka pia ilikiuka haki za kibinadamu katika vita hivi vyake na Tamil Tigers.


Kwa miongo mitatu Prabhakan alimudu kuongoza kundi kubwa la wapiganaji wa Kitamil waliokuwa watu wa kwanza kutumia mbinu ya kujilipua kwa kujitoa mhanga. Watu mashuhuri wanaosemekana waliuawa kwa amri ya Prabhakan ni rais wa zamani wa Sri Lanka Ranasinghe Premadasa mwaka wa 1993. Mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu wa India Rajiv Gandhi mwaka wa 1991 pia yanasemekana yalitekelezwa kwa amri ya Prabhakan. Gandhi aliingia katika daftari baya la Prabhakan alipotuma wanajeshi wa India kupambana na Tamil Tigers mwaka wa 1987.


Mwandishi: Munira Muhammad/ afp

Mhariri: Mohammed Abdulrahman