1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steimeier aitolea wito Qatar kuheshimu wafanyakazi

2 Juni 2014

Waziri wa Mambo wa Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amekuwa ziarani Mashariki ya Kati na Ghuba ya Arabuni alikowatembelea wakimbizi wa Syria na Qatar, taifa muhimu kwa siasa za nje za Magharibi.

https://p.dw.com/p/1CAPE
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Qatar, Khalid al-Attiyah, mjini Doha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Qatar, Khalid al-Attiyah, mjini Doha.Picha: picture-alliance/dpa

Kuwasili kwa Steinmeier mjini Doha hapo jana, kulisadifiana na kutangazwa kwa makubaliano ya mabadilishano ya wafungwa kati ya Marekani na kundi la wanamgambo wa Taliban la Afghanistan, ambayo yamesimamiwa na Qatar.

Lakini kama kawaida, ishara ya namna mataifa ya Magharibi yanavyofanya kazi na taifa hilo dogo na tajiri kwenye Ghuba ya Arabuni, na hatua kubwa ya kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa hilo, ilitiwa ukungu na madai ya Qatar kuwatendea visivyo wafanyakazi wa kigeni.

Katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Khalid al-Attiyah aliahidi kuyashughulikia masuala yote kuhusiana na hali za wafanyakazi waliokuwa wakisaidia kuitayarisha Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022.

“Tuna dira ya 2030 na sio tu Kombe la Dunia la 2022. Tunaangazia mbali zaidi ya hapo. Bado tuna dhamira ya kweli ya kurekebisha makosa, kama yapo.“ Alisema Attiyah.

Baada ya kushinda haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2010, taifa hilo dogo na tajiri lenye wakaazi milioni 2 na laki moja tu, lilitangaza mipango ya ujenzi wa miradi na miundombinu kwa miaka 15 ijayo.

Lakini hali za wafanyakazi wa ujenzi nchini humo zilifahamika pale gazeti la Guardian la Uingereza liliporipoti mnamo mwezi Septemba juu ya maelfu ya wafanyakazi kutoka Nepal ambao walikuwa hawapewi chakula wala maji ya kutosha.

Mgongano juu ya Syria

Tafauti nyengine ni msimamo wa Qatar kuunga mkono waasi wenye mafungamano na dini ya Kiislamu nchini Syria. Katika baadhi ya maeneo, makundi hayo, kama lile la Ahfad al-Rasul, yanapigana dhidi ya Jeshi Huru la Syria, ambalo linaungwa mkono na wale wanaoitwa Marafiki wa Syria, ambao wanazijumuisha Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na hata Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar yenyewe. Waziri Steinmeier aliwaambia waandishi wa habari hili litawekwa sawa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akiwa na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Tarid el-Zaid mjini Doha, Qatar.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akiwa na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Tarid el-Zaid mjini Doha, Qatar.Picha: picture-alliance/dpa

“Hapana shaka tulikuwa na mazungumzo na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim al-Thani na pia Waziri wa Mambo ya Nje, Khalid al-Attiyah, juu ya Syria. Tulishatumia takribani nusu nzima ya siku kuzungumzia msaada kwa makundi yenye msimamo wa wastani kwenye mkutano wa London.” Alisema Steinmeier.

Hata hivyo, kuna ambalo mawaziri hao wawili wa mambo ya nje walikubaliana kuhusu Syria, nalo ni kutokuukubali uchaguzi wa rais unaofanyika kesho nchini Syria. Kuwe na kusiwe na uchaguzi, anasema Steimeier, lazima mataifa washirika yakae tena kuzungumzia suluhisho la kisiasa la Syria.

Mwandishi: Dagmar Engel
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman