1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier Afghanistan

Kalyango Siraj25 Julai 2008

Atakabidhi mradi wa maji safi Herat kwa wenyewe

https://p.dw.com/p/EjYt
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier yuko nchini Afghanistan kwa ziara rasmi ya siku nne.

Hii ni zaira yake ya tatu nchini humo ambapo majeshi ya Ujerumani yanasaidia kukarabati miundo mbinu ilioharibiwa na vita vya mda mrefu.

Bw Steinmeier kwa sasa yuko katika mji wa Herat unaopatikana katika sehemu ya magharibi ya taifa hilo ambalo limezongwa na vita. Kutokana na hali hiyo ziara yake hii haikutangazwa.Na atakuwa nchini humo kwa mda wa siku nne.

Taarifa iliotolewa na wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani mjini Berlin imesema kuwa waziri Steinmeier akiwa huko Afghanistan miongoni mwa mengine atakabidhi mradi wa maji safi kwa watawala wa Afghanistan. Mradi huo utawasaidia wakazi wa mji huo wanaokisiwa kuwa nusu millioni, na kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mashauri ya nje mradi huo ulianzishwa kwa msaada wa Ujerumani.

Aidha Bw Steinmeier anatarajiwa kufanya mazungumzo na maafisa wa eneo hilo pamoja na wa mji huo kabla ya kukutana na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Herat.

Taarifa atakazokusanya huko kwa upande mmoja zitatumiwa kutayarisha uamuzi wa bunge la Ujerumani mwezi Oktoba ili kutilia nguvu hoja za kuweza kulishawishi bunge kukubali vikosi vyake kurefusha mda wake nchini Afghanistan.

Kwa upande mwingine Ujerumani inakabiliwa na shinikizo la kuongeza idadi ya vikosi vyake nchini Afghanistan na pia kuvituma sehemu tete za kusini mwa nchi hiyo kutoka sehemu tulivu za kaskazini.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema wazi kuhusu suala hilo akisisitiza kuwa sera kuhusu shughuli za kijeshi za vikosi vyake nje ya nchi hazikubali kuongezea.

Akizungumza kabla ya ziara ya seneta wa Marekani Barak Obama.Merkel alisema kuwa lazima kuwe na mezania sawa kati ya shughuli za kijeshi pamoja na matarajio ya kisiasa ya serikali ya Afghanistan.

Mbali na hayo serikali ya Ujerumani, mwezi jana ilitangaza kuongeza askari zaidi sehemu za kusini baadae mwaka huu.Iliahili kuongeza askari wengine 1,000 na hivyo kufikia elf nne na mia tano.

Hata hivyo wazo hilo la kuongeza wanajeshi pamoja na kuwatuma katika eneo la kusini linalotokota linapingwa sana hapa Ujerumani,linaweza kusababisha matatizo wakati wa uchaguzi.

Sehemu za kusini za Afghanistan ndiko vikosi vya ushirika wa NATO vinapambana na wapiganaji wa Kitaliban.Huku kwa upande mmoja majeshi ya Ujerumani kikatiba hayaruhusiwi kushiriki katika mapigano nje ya nchi.

Suala la majeshi likiwa tete lakini la kusaidia ukarabati laonekana halina matatizo.

Kwani Ujerumani,imeahidi kutoa msaada wa thamani ya Euro zaidi ya billioni moja hadi mwaka wa 2010 kwa ajili ya ukarabati na kuiendeleza Afghanistan.