1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier aikosoa 'barua kwa Iran'

Mohammed Khelef13 Machi 2015

Ujerumani inaikosoa "Barua kwa Iran" iliyoandikwa na wabunge 47 wa chama cha Republican, huku wabunge hao wakisema wanasimamia walichokiandika kwenye waraka huo uliozuwa utata.

https://p.dw.com/p/1EqBh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na mwenzake wa Marekani, John Kerry, mjini Washington.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na mwenzake wa Marekani, John Kerry, mjini Washington.Picha: Reuters/Y. Gripas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ambaye yuko ziarani nchini Marekani, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kinachoweza kufanywa pekee na barua hiyo ya maseneta wa Republican ni kuiambia Iran kwamba mataifa ya Magharibi hayawezi kuaminika.

Katika mkutano huo kabla ya kukutana na wabunge kwenye jengo la Capitol Hill siku ya Alhamisi, Steinmeier alisema kilichofanywa na wabunge hao 47 hakina manufaa kwa mchakato wa kimataifa, ambao hauhushishi Marekani pekee.

"Sasa Iran inaweza kutugeukia kutuambia: je kweli nyinyi munaaminika kwa ahadi munazotoa ikiwa maseneta 47 wanasema chochote kinachokubaliwa na serikali, hatimaye wao watakifuta? Hili si jambo la siasa za ndani tu za Marekani, bali ni jambo lenye athari kwenye mazungumzo tunayoyafanya Geneva," alisema waziri huyo wa mambo ya nje ambaye aliongeza kuwa barua hiyo "haiusaidii mtazamo wa makubaliano ambayo hayataweza kufikiwa kirahisi."

Steinmeier alisema ingawa hali ya kutokuaminiana ipo kati ya pande zinazoshiriki mazungumzo hayo, lingelikuwa jambo jema kama barua hiyo ya maseneta haitasababisha tena madhara kwenye mazungumzo hayo.

McCain ajitetea

Hata hivyo, seneta wa ngazi za juu wa chama cha Republican, John McCain, na ambaye ni mmoja wa waliosaini barua hiyo ya Seneta Tom Cotton, alimkosoa Waziri Steinmeier kwa kauli yake hiyo, akisema waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani hana mamlaka yoyote ya kuzungumzia barua hiyo.

Seneta John McCain.
Seneta John McCain.Picha: Reuters

"Ni kweli ingelikuwa vyema kama tungelikaa tukajadiliana zaidi kuhusu barua ile, lakini hatukuwa na wakati huo na sijutii sasa kwa kuisaini." Alisema McCain, ambaye badala yake alimlaumu Steinmeier na serikali nzima ya Ujerumani katika suala jengine la mzozo wa Ukraine, ambao alidai Ujerumani inazuia kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya Rais Vladimir Putin wa Urusi aliyedai anawauwa raia wa Ukraine kila siku.

Barua hiyo ya maseneta wa Republican imeikasirisha Ikulu ya Marekani na pia kukosolewa vikali na vyombo kadhaa vya habari ndani na nje ya Marekani, wanaowatuhumu maseneta hao kuvunja sheria za Marekani kwa kuwasiliana na serikali za kigeni bila kupitia serikali yao.

Hapo jana kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alisema anatiwa hofu na Marekani kwani taifa hilo ni mashuhuri kwa tabia ya kuwachoma wengine visu vya mgongo, akikusudia kusaliti makubaliano yanayofikiwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba