1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier akamilisha ziara yake barani Afrika

Ummilkheir14 Februari 2008

Kiongozi huyo alizitembelea Ghana, Togo na Burkina Faso

https://p.dw.com/p/D7Tf
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akilakiwa na mwenzake wa Burkina Faso Djibrill Yipãnã Bassolé, katika uwanja wa ndege wa mjini OuagadougouPicha: picture-alliance/ dpa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amemaliza ziara ya siku tatu katika nchi za Afrika magharibi.

Baada ya kuitembelea Ghana ambako alishuhudia pia fainali ya kombe la mataifa barani Afrika, alielekea Togo, ambako mbali na mazungumzo ya kisiasa, alikifungua pia kituo cha kupambana na maradhi ya nchi za joto. Kituo cha mwisho cha ziara yake barani Afrika ni Burkina Fasso.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinemeier hakutarajia kabisa kama angepokelewa kwa shangwe na sherehe kubwa kama zile alizozishuhudia. Alipoteremka toka ndani ya gari yake huko Tsevié, alikuta umati wa wakaazi wa mji huo wamekusanyika kumkaribisha kwa muziki, densi na sherehe nyingi nyengine za mapokezi.

Steinmeier amefika mjini humo kwaajili ya kufungua kituo cha tiba ya maradhi ya nchi za joto kinachogharimiwa kikamilifu na Ujerumani. Baada ya kupeana mikono na watu chungu nzima na kuketi baadae mbele ya jengo la kituo hicho, alikaribishwa kwa hotuba iliyotolewa kwa kijerumani na waziri wa afya wa Togo Kondi Charles Akba.

"Mungu ibariki Ujerumani, Mungu ibariki Togo, Mungu aubariki ushirikiano kati ya Ujerumani na Togo."

Katika kituo hicho kipya cha huduma za afya,watu watakua wakitibiwa maradhi ya Buruli-maradhi hatari ya nchi za joto ambayo hayajulikani vyema bado kwa wakati huu.

Sherehe za ufunguzi zilikua za aina pekee kwa namna ambayo itifaki zote za kibalozi ziliachwa kando.Steinmeier anasema:

"Sikutegemea hata kidogo kuona hali ya urafiki kama hii,na jinsi lugha ya kijerumani inavyowavutia watu. Kuna wanafunzi zaidi ya 800 wa chuo kikuu wanaosomea lugha na utamaduni wa Ujerumani, kuna maelefu ya wanafunzi wanaojifunza lugha ya kijerumani shuleni. Hali hiyo pekee inadhihirisha uhusiano wa dhati ulioko kati ya Ujerumani na Togo na inadhihirisha pia matarajio ya kizazi kipya kuona uhusiano huu wa jadi unaendelezwa."

Kwa miaka kadhaa uhusiano kati ya Ujerumani na Togo ulikua umepooza kutokana na utawala wa kiimla uliokuwepo madarakani na kung'atuka baada ya machafuko ya umwagaji damu ya mwaka 2005. Hali ni shuwari hivi sasa na Togo imeanza kufuata ujia wa demokrasia.

Katika mazungumzo yake pamoja na rais wa Togo na viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo,waziri wa mambo ya nchi za nje Steienmeier amehimiza juhudi za kidemokrasi ziendelezwe na kutendelea pia kufanyiwa marekebisho taasisi za nchi hiyo.

Mbali na wanasiasa,waziri wa mambo ya nchi za anje wa Ujerumani Frank Walter Steienmeier alikutana pia na wanaharakati wa haki za binaadam waliosifu mchango wa Ujerumani katika juhudi za kuimarisha demokrasia nchini mwao.