1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za ghuba zaombwa kuwapokea wakimbizi zaidi

Admin.WagnerD19 Oktoba 2015

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Steinmeier ametoa wito kwa Saudi Arabia na mataifa mengine ya ghuba kuchukua hatua zaidi kwa ajili ya mamia kwa maelfu ya watu wanaokimbia vita na ghasia katika mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/1GqYo
Steinmeier in Saudiarabien
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Steimeier na waziri wa mambo ya kigeni wa saudi Arabia al-FaisalPicha: AP

Tunataka eneo lote katika ghuba ya Arabuni kushiriki katika kuwapatia msaada wakimbizi, Steinmeier amesema kufuatia mazungumzo na mfalme wa saudi Arabia Salman mjini Riyadh.

Steinmeier , ambaye yuko katika ziara ya siku nne katika eneo hilo la ghuba, amesema hii ni pamoja na kuwachukua wakimbizi. Mataifa tajiri ya ghuba yamekabiliwa na ukosoaji kwa kusita kwao kuwapokea wakimbizi wa Syria.

Aussenminister Frank Walter Steinmeier und Prinz Saud al-Faisal bei einer Pressekonferenz in Saudi Arabien am 28.10.2008
Waziri Steinmeier na mwanamfale Saud al- FaisalPicha: AP

Mataifa ya ghuba yanasema yamechukua mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Syria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vianze mwaka 2011, ikiwa ni pamoja na wakimbizi nusu milioni nchini Saudi Arabia na laki moja katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Wakati huo huo maelfu ya wahamiaji wameendelea kumiminika leo katika mataifa ya Balkan, ambako udhibiti mkubwa wa mipaka umesababisha mlundikano wa wahamiaji, wengi wao wakikimbia vita nchini Syria , Iraq na Afghanistan, wakisafiri kupitia Uturuki, Ugiriki na mataifa ya Balkan magharibi, wakiwa na matumaini ya kupata usalama nchini Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya.

Slowenien Kroatien Flüchtlingskrise
Mzozo wa wakimbizi SloveniaPicha: Reuters/A. Bronic

Wakimbizi wazidi kuingia Ulaya

Wimbi jipya limeingia Macedonia kutoka Ugiriki mwishoni mwa juma, wakati watu 10,000 wanavuka na kuingia katika nchi hizo katika muda wa saa 24 zilizopita, polisi imesema.

Lakini hali ya wasi wasi imeongezeka zaidi katika njia wanayopitia wakimbizi baada ya Hungary kufunga mpaka wake kwa uzio wa waya, na kusababisha mmiminiko huo wa wahamiaji kuelekea upande wa magharibi kuelekea Slovenia, ambayo nayo imeweka ukomo kwa watu wanaowasili.

Slowenien Kroatien Flüchtlingskrise
Wakimbizi wakiwa nchini SloveniaPicha: Reuters/S. Zivulovic

Slovenia leo imekataa kuwaruhusu wahamiaji zaidi ya 1,000 wanaowasili kutoka Croatia, wakisema kiwango cha ruhusa ya kuingia kwa siku kimefikiwa.

Hatua hiyo imeongeza hofu ya mkusanyiko mkubwa wa watu, wakati treni iliyowabeba watu 1,800 ikiwasili usiku katika upande wa pili wa mpaka wa Croatia , lakini ni watu 500 tu , wale ambao wanaweza kukabiliwa haraka na matatizo , wengi wakiwa wanawake na watoto, wakiruhusiwa kuvuka mpaka, polisi imesema.

Misururu mirefu

Misururu mirefu pia ilionekana katika upande wa mpaka kati ysa Serbia na Croatia, ambako mamia walilala usiku kucha wakinyeshewa na mvua na baridi kali.

Kansela wa Ujerumani wa Ujerumani amesema tatizo la wakimbizi ni lazima lipatiwe ufumbuzi na mataifa ya Ulaya na jumuiya ya kimataifa.

"Kupambana na wimbi kubwa kabisa duniani la wakimbizi tangu vita vikuu vya pili vya dunia ni tatizo la dunia na linaweza tu kushughulikiwa kwa mtazamo wa pamoja wa mataifa ya Ulaya na dunia kwa jumla."

Deutschlandtag der Jungen Union - Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Lengo la wengi wa wahamiaji hao ni nchi yenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya , Ujerumani, ambayo inatarajia kuwachukua karibu wakimbizi milioni moja mwaka huu, na ambako sera za kansela Angela Merkel za kuweka milango wazi zimezusha shutuma nyingi dhidi yake.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Yusuf , Saumu