1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier: Mkataba wa Minsk unapaswa kuendelea

15 Agosti 2016

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amesema mkataba wa Minsk unapaswa kubakia lengo kuu mchakato wa amani ya Ukraine, licha ya mvutano uliopo katika eneo la Crimea ambalo lilitwaliwa na Urusi.

https://p.dw.com/p/1JiPb
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/D. Sorokin

Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi-RIA, Steinmeier ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waziri mwenzake wa Mambo ya Nchi za Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Wanadiplomasia hao wamekutana kwenye mji wa Yekaterinburg, Urusi baada ya Rais wa Urusi, Vladmir Putin kuituhumu Ukraine kwa kutumia mbinu za kigaidi kujaribu kuanzisha mzozo mpya na kuondoa hali ya utulivu kwenye eneo la Crimea. Tuhuma ambazo hata hivyo, Ukraine imezikanusha.

RIA imemnukuu Steinmeier akisema kwamba Mkataba wa Minsk unapaswa kuendelea kuwa lengo kuu katika mchakato. Aidha, Lavrov ameahidi kwamba Urusi itatekeleza sehemu yake kulingana na mkataba huo. Urusi imekuwa ikiishutumu Ukraine kwa kutoheshimu majukumu yake chini ya mkataba huo wa amani.

Lavrov amefafanua kwamba hadhani kama kuna mtu yeyote ambaye anakusudia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Ukraine. Amesema Urusi iko tayari kuonyesha ushahidi kuhusu madai ya kuidhibiti Crimea, kwa washirika wake wa Magharibi.

Steinmeier aisihi Urusi kusitisha mapigano Aleppo

Ama kwa upande mwingine, Waziri Steinmeier ameitolea wito Urusi kuweka chini silaha ili kuruhusu misaada ya kibinaadamu kuufikia mji unaokabiliwa na vita wa Aleppo uliopo kaskazini mwa Syria. Kauli hiyo ameitoa leo kabla ya kukutana na Lavrov ambapo amesisitiza ni lazima mapigano yasitishwe ili watu waweze kupatiwa mahitaji muhimu.

Eneo la kizuizi Aleppo
Eneo la kizuizi AleppoPicha: picture-alliance/Sputnik/M. Alaeddin

Wiki iliyopita, Urusi ambayo ni mshiriki muhimu wa serikali ya Syria, ilitangaza kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu ili kuruhusu misaada ya kibinaadamu kuingia Aleppo. Lakini Umoja wa Mataifa umesema hatua hiyo haikuzaa matunda. Lavrov amesema wanamgambo wa Syria wanatumia mwanya wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kujidhatiti zaidi na kuimarisha vikosi vyao.

Kwa pamoja, Steinmeier na Lavrov, wamekiri kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Ujerumani umedhoofika kwa sasa. Hata hivyo, Steinmeier amesema ana imani uhusiano huo utarejea katika hali yake ya kwaida hivi karibuni, akiongeza kusema kuwa Ujerumani ni mshirika muhimu wa kimkakati wa Urusi.

''Baada ya yale yaliyotokea Ukraine, uhusiano wetu umerudi nyuma, lakini licha ya hayo, lazima tuendeleze mazungumzo na kujihusisha na juhudi zote za kuitatua hali hii,'' amesema Steinmeier.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliingia dosari baada ya Urusi kuidhibiti Rasi ya Crimea mwanzoni mwa mwaka 2014, baada ya Ukraine kumuondoa madarakani rais aliyekuwa akiungwa mkono na Urusi, pamoja na ushiriki wa Urusi katika mapigano ya mashariki mwa Ukraine.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters,DPA
Mhariri: Mohammed Khelef