1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeir aelezea matumaini yake kwa Lebanon baada ya kukutana na rais mpya wa nchi hiyo.

Mohamed Dahman1 Juni 2008

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeir amewaambia waadishi wa habari kwamba ameona dalili za matumaini nchini Lebanon baada ya kukutana na rais mpya aliechaguliwa hivi karibuni Michel Suleiman.

https://p.dw.com/p/EAmp
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, kulia, akipeana mkono na Rais mpya wa Lebanon Michel Suleiman, kushoto, katika jumba la rais huko Baabda karibu na Beirut nchini Lebanon Jumapili ya tarehe Mosi Juni mwaka 2008.Picha: AP

Steinmeir amesema makubaliano ya Doha kati ya makundi ya Lebanon yaliomaliza mzozo wa miezi 18 wenye madhara kwa nchi hiyo ni hatua muhimu sana kukomesha mzozo huo.

Amesema kuchaguliwa kwa rais na kuundwa kwa serikali ni ishara za matumaini akisisitiza kwamba makubaliano hayo yanasema kwamba nguvu na silaha hazipaswi kutumiwa kututawa mzozo huo.

Steinmeir ameongeza kusema kwamba ni jambo la kutia moyo kwamba katika hotuba ya kuapishwa kwake Suleiman ameelezea kuunga mkono mahkama ya kimataifa kuwashtaki waliohusika na mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri na viongozi wengine wanaoipinga Syria.

Pia amesisitiza kwa nchi jirani ya Syria kutambuwa uhuru wa Lebanon kuanzia hivi sasa.

Beirut ni kituo cha kwanza cha ziara ya Mashariki ya Kati ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ambayo pia itamfikisha Jerusalem nchini Israel na Ramalla Ukingo wa Magharibi.