1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeir akabiliwa na majukumu magumu katika chama cha SPD

Charo, Josephat8 Septemba 2008

Steinmeier na Münterfering wanalazimika kushirikiana kukiokoa chama cha SPD

https://p.dw.com/p/FDhf
Mwenyekiti wa chama cha SPD Franz Muentefering (kushoto) na mgombea ukansela wa chama hicho Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Chama cha SPD kinataka kuingia katika uchaguzi ujao na Frank Walter Steinmeier akiwa mgombea wake wa ukansela wa Ujerumani na Franz Müntefering kama mwenyekiti wa chama. Hivyo basi mivutano ndani ya chama hicho bado haijatatuliwa.

Baada ya kipindi kirefu cha vuta ni kuvute kuchaguliwa kwa Frank Walter Steinmeietr kugombea ukansela wa Ujerumani kwa tiketi ya chama cha Social Democratic, SPD, kunatakiwa kupunguza hali ya kutoelewana katika chama hicho. Lakini wakati huo huo, wadhifa wa uenyekiti wa chama cha SPD ambao ulikuwa ukishikiliwa na bwana Kurt Beck sasa umechukuliwa na bwana Franz Münterfering ambaye kwa kipindi ambacho hakijatimia miaka mitatu aliagwa baada ya kikitumikia chama hicho.

Münterfering kama mwenyekiti wa chama cha SPD alikiongoza chama hicho kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kansela wa zamani Gerhard Schroeder. Mnamo mwaka wa 2004 wakati Schroder alipoacha kuwa mwenyekiti wa chama ili kuuokoa wadhifa wake wa ukansela, bwana Franz Münterfering alichukua majukumu ya uenyekiti wa chama cha SPD.

Mwaka mmoja na nusu baadaye, baada ya kansela Schroder kushindwa kwenye uchaguzi mkuu na kansela wa sasa Bi Angela Merkel, Andrea Nahles aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha SPD ingawa bwana Franz Münterfering hakutaka iwe hivyo. Hatua hii ilimfanya Münterfering kujiondoa chamani.

Kama suluhu kwa tatizo lililosababishwa na kuondoka kwa bwana Franz Münterfering, waziri kiongozi wa jimbo la Brandenburg, Matthias Platzeck, alichaguliwa kukiongoza chama cha SPD, lakini kutokana na hali mbaya ya afya yake, akalazimika kuacha kazi ya kukiongoza chama. Bahati ya kukiongoza chama cha SPD ikamuangukia bwana Kurt Beck, ambaye alikuwa ameshinda kwa kishindo uchaguzi wa jimbo la Rheinland-Pfalz.

Ukweli ni kwamba chama cha SPD kimerudi nyuma chini ya uongozi wa bwana Beck na kiongozi huyo alifanya makosa kadhaa ya kibinafsi. Pia bwana Beck hakuweza kuzuia kushuka kwa umaarufu wa chama cha SPD humu nchini.

Wanasiasa hawa waili, Frank Walter Steinmeier na Franz Münterfering wanatakiwa sasa kukiokoa chama cha SPD, ambacho uongozi wake wa ndani hauna umaarufu mkubwa. Muungano wa vyama vya Christian Social Union, CSU na Christian Democtaic Union, CDU, unatakiwa kunufaika, lakini bado kumesalia mwaka mmoja hivi kabla uchaguzi mkuu kufanyika hapa Ujerumani. Kuna mda mrefu wa migogoro ndani ya chama na kwa hiyo Steinmeier na Münterfering wanalazimika kushirikiana kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, la sivyo wahatarishe nafasi ya chama kushinda uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa kura ya maoni ya hivi karibuni, mwisho wa chama cha SPD kuwa chama kinachopendwa na wananchi hauko mbali tena. Bwana Frank Walter Steinmeier kama mwanasiasa mahiri na kiongozi anayeibeba bendera ya chama cha SPD kuelekea uchaguzi mkuu hapa Ujerumani, bila shaka anakabiliwa na kibarua kigumu.