1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeir akamilisha ziara Afrika.

Utte Schaeffer/Prema Martin4 Agosti 2007

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier akiendelea na ziara yake ya Afrika ya Magharibi,hii leo atakuwa na majadiliano mengine ya kisiasa katika mji mkuu wa Ghana,Accra.

https://p.dw.com/p/CB2F
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani akiwa na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Nigeria Bagudu Hirse mjini Abuja,Nigeria.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani akiwa na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Nigeria Bagudu Hirse mjini Abuja,Nigeria.Picha: AP

Ziara iliyoanzia nchini Nigeria siku ya Jumatano na kumalizika leo hii nchini Ghana imempeleka Waziri wa Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier,nchi mbili muhimu katika Afrika ya Magharibi.Baada ya kukutana na Rais Umaru Yar Àrdua wa Nigeria aliechaguliwa hivi karibuni, Steinmeier alisema ameridhika mno na majadiliano yao.Hata hivyo,Nigeria pia hudhihirisha kwamba utaratibu wa kidemokrasia na vita dhidi ya rushwa hujikuta katika njia ngumu.

Ameongeza kusema kwamba ni matumaini yake kuwa rais mpya alieingia madarakani na mradi wenye malengo makuu,hasa kuendeleza utawala wa kisheria na kupiga vita rushwa atafanikiwa.Na kwamba kazi zake hazitozuiliwa na makundi yasiokuwa labda na hamu kwa hivi sasa.

Pande zote mbili zilikubaliana kuwa mkutano wa kilele kati ya Ulaya na Afrika unaotazamiwa kufanywa mwezi wa Desemba,ni nafasi nzuri ya kujadili masuala muhimu ya kisiasa na kujaribu kubadilishana maoni baada ya kutokuwepo mkutano wa aina hiyo tangu zaidi ya miaka sita.Nigeria sawa na Ujerumani zina hamu ya kuendeleza uhusiano wao.Nigeria ingependa kushiriki zaidi katika uchumi wa Ujerumani,hasa katika sekta ya nishati.

Kwa upande wake,Steinmeier ambae hakufuatana na tume ya wataalamu wa kiuchumi na wakati wa ziara yake ametoa kipaumbele kujenga mahusiano ya kitamaduni na kisiasa,alipendekeza kubadilishana zaidi wataalamu wa kiuchumi na wanafunzi na vile vile kuongeza misaada ya kulipia masomo ya wanafunzi wa Kiafrika.

Migogoro kama vile ya hivi sasa nchini Sudan na Somalia hudhihirisha umuhimu wa mataifa ya Kiafrika kufanya kazi pamoja kwa haraka na mafanikio zaidi kuliko hapo awali,ili kuzuia na kutenzua mizozo hiyo.

Steinmeier katika majadiliano yake pamoja na viongozi wa Kiafrika,wamekubaliana juu ya umuhimu wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,kilichoidhinishwa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa kwenda kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan.Nigeria na Ghana mara kwa mara zimehimiza utaratibu huo na hushiriki katika juhudi za kuleta usalama na utulivu barani Afrika.Kwa sababu hiyo pia inapasa kuendeleza ushirikiano pamoja na nchi hizo katika siku zijazo.