1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Strauss-Kahn aachiliwa kwa dhamana

Halima Nyanza20 Mei 2011

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani -IMF- Dominique Strauss-Kahn ambaye anatuhumiwa kwa tuhuma za kujaribu kubaka anaachiliwa huru leo kwa dhamana.

https://p.dw.com/p/11KCB
Dominique Strauss-KahnPicha: AP

Jaji wa mahakama ya New York Michael Obus aliagiza Dominique Strauss-Kahn kuachiliwa mapema leo kwa masharti ya kutoa dhamana ya fedha taslim, dola milioni moja na bima ya dola milioni 5, kuvaa kifaa maalumu cha umeme kuchunguza mienendo yake, kukabidhi hati zake zote za kusafiria na kuishi katika kizuizi cha nyumbani kwa saa 24.

Kulingana na masharti hayo, inamaanisha kuwa mwanasiasa huyo wa Kifaransa, ambaye amejiuzulu katika wadhfa wake huo wa Ukurugenzi wa IMF, ataondoka katika maeneo yenye ulinzi mkali jirani na gereza la kisiwa cha Rikers na kuungana  na mke wake Anne Sinclair na binti yao Camille ambao wote walikuwepo mahakamani jana.

Aidha  katika nyumba atakayokuwa akiishi pia atakuwa na uwezo wa kuwasiliana na mawakili wake kuandaa utetezi wake bila ya mipaka yoyote.

Amefunguliwa rasmi mashtaka saba ya uhalifu wa kingono yanayohusiana na jaribio lake la kutaka kumbaka mhudumu wa hoteli ya Manhattan Jumamosi iliyopita.

Wakati huohuo, kashfa inayomkabili mkuu huyo wa zamani wa IMF na hatua yake ya kujiuzulu imeongeza mivutano duniani kote juu ya mtu atakayechukua nafasi hiyo, katika kipindi ambacho Shirika hilo la Fedha la kimataifa likiwa katika mazungumzo nyeti kuhusiana na mzozo wa madeni uliozikumba nchi zinazotumia sarafu ya Euro.

Lakini hisia zisizoepukika zimeongezeka kwamba bara la Ulaya litabaki kuishiklilia nafasi hiyo, huku Waziri wa Fedha wa Ufaransa Christine Lagarde akionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa.

Akiunga mkono hilo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia anataka tena mtu kutoka barani Ulaya kuongoza chombo hicho.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha wa Marekani Timothy Geithner ametaka mchakato wa wazi utakaoongoza utaratibu wa kumpata mtu atakayechaguliwa.

Vyanzo vya habari kutoka Washington, vinasema kuwa Marekani ambayo ni mchangiaji mkubwa wa fedha katika taasisi hiyo itaiunga mkono Ulaya katika kumpata mtu atakayerithi nafasi hiyo.

Suala hilo inawezekana likajadiliwa katika mkutano wa viongozi wa kundi la nchi nane zilizoendelea kiviwanda linalojulikana kama  G8, utakaofanyika nchini Ufaransa wiki ijayo.

Kwa pamoja Marekani na mataifa ya Ulaya yanashikilia zaidi ya nusu ya kura na hivyo kuwa na sauti ya nani atakayeiongoza taasisi hiyo ya fedha.

Katika hatua nyingine, China, iimeunga  mkono miito ya mataifa ya bara la Asia kutaka kiongozi mpya wa IMF achaguliwe kutoka taifa linaloinukia kiuchumi.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, AFP)

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman