1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stuttgart yaitimua Hertha Berlin kileleni ?

23 Machi 2009

Mwanya wa pointi 4 iliokua nao Berlin kileleni umenywea hadi pointi1:

https://p.dw.com/p/HI00
Sami Khedira (Stuttgart) atia bao lango la BerlinPicha: AP

Mabingwa wa Uingereza, Manchester United wateleza tena kileleni mwa Premier League kwa kukandikwa mabao 2:0 na Fulham, Steven Gerrad wa Liverpool, ameoinya Manu kuwa Liverpool itatoroka na kombe-Hertha Berlin, inaongoza bado Bundesliga, lakini mwanya wake wa pointi 4 kileleni umepunguzwa na mabingwa Bayern Munich na Wolfsburg hadi pointi 1-je, nani ataibuka msimu huu bingwa ?

Hertha Berlin imekandikwa mabao 2-0 wakati mabingwa Bayern Munich na Wolfsburg,wote wameshinda. Munich waliitimua nje Karslruhe inayoburura mkia wa Ligi ingawa kwa bao 1:0 -bao la Jose Sosa .Sasa Munich inanyatia kushikma usukani wa ligi mwishoni mwa wiki ijayo.

Wolfsburg nayo ikitamba na mshambulizi kutoka Brazil Grafete,imenyakua ushindi wake wa 7 mfululizo ilipoizaba Armenia Bielefelfd mabao 3-0. Hertha ina pointi 49 na Bayern Munich na Wolfsburg ziko nafasi ya pili kwa pionti sawa 48.Munich na Wolfsburg kwahivyo, zitaoneshana wiki mbili kutoka sasa nani ashike usukani wa Ligi.Stuttgart ilifuta madhambi yake ya kuchapwa mabao 4-0 na Bremen mwishoni mwa wiki iliopita, kwa kuitandika Hertha Berlin mabao 2-0 kufuatia kipindi cha mapumziko.Mshambulizi wao Andrey Veronin mara hii hakufua dafu.Cacau kutoka Brazil alipioga hodi katika lango la Berlin na kukaribishwa ndani kwa bao la kwanza.Sami Khedira akalifumania lango la Berlin kwa bao la pili na la mwisho dakika 5 baadae alipoutia kichwa mpira kutokana mkwaju aliouchapa Hitzlperger.

Ushindi huo unaipachika Stuttgasrt nafasi ya 6 ya ngazi ya ligi na kuweza kuania alao nafasi ya kucheza champions League au kombe la ulaya la UEFA.Baada ya kulia firimbi ya mwisho, kocha wa Hertha Berlin kutoka Uswisi alisema:

"Wenzetu walicheza bora zaidi.Zilikuwa timu 2 tofauti uwanjani leo-moja ilicheza uziri kabisa na nyengine ilicheza vibaya. Sio kusema sijaridhika sana ,lakini ukizabwa mabao 2:0 ,ukiwa kocha unabidi uridhie ,lakini haukuwa kabisa wa kuridhisha."

Mbrazil Grafite alietia bao lake la 18 katika mechi 16 pale Wolfsburg ilipoitembelea Bielefeld jumamosi.Kwa ushindi wa mabao 3-0 ,Wolfsburg imetoa salamu kwa Berlin,Hamburg na Munich kuwa huu huenda pia ukawa msimu wao wa kutwaa kombe,kwani katika safu yao wana mbrazil Grafite.Selim Teber amewapa chipukizi Hoffenheim bao la kwanza walipopambana na Hannover,lakini mwishoe, timu hizo mbili ziliachana suluhu 2:2.Hoffenhewim sasa imeangukia nafasi ya 5 baada ya kuanza mwaka mpya ikiwa kileleni.

Cottbus,iko bado hatarini ya kurudi daraja ya pili baada ya kukomewa nyumbani mabao 2:0 na FC Cologne.Nahodha wa FC Cologne,mslovenia Novakovic alitia mabao yote 2 ya timu yake.Bayer Leverkusen yenye miadi na jirani zao Cologne mwishoni mwa wiki ijayo, walitoka suluhu ya bao 1:1 na Frankfurt.

Ama katika changamoto za Premier League-Ligi ya Uingereza, kinyanganyiro cha kombe hilo sasa kiko wazi baada ya mabingwa Manchester united kuongoza kwa muda mrefu.Manu imelazwa kwa mara ya pili mfululizo mara hii na Fulham kwa mabao 2:0.Kwanza, ilichezeshwa kindumbwendumwe na Liverpool ilipochapwa mabao na sasa stadi wake Steven Gerrad alietia mabao 3 kati ya mabao 5 katika lango la Aston Villa jana, ameionya Manchester ikiendelea kupoteza pointi, mwishoe watalikuta taji si lao.

Manchester united hatahivyo, inaongoza Orodha ya Ligi ikiwa na jumla ya pointi 65,hivyo ina pointi 1 tu zaidi kuliko FC Liverpool.Chelsea nayo imeteleza ilipokandikwa bao 1:0.

Katika La Liga, ligi ya Spian FC Barcelona ya mkamerun samuel Eto-0 imerudi kutamba kwa kuitimua nje Malaga jana kwa mabao 6:0 (bila majibu).

Sasa Barcelona inaendelea kuongoza Ligi ya Spian kwa pointi 6 na hivyo imehakikisha hakuna mabadiliko kati ya timu 4 za kileleni mwa Ligi.Real Madrid inanyatia kutoka nafasi ya pili. Mkamerun samuel eto-o alitia mabao 2 kati ya hayo 6 ya Barcelona. Real Madrid iliikomea Almeira mabao 3-0

Mwandishi.Ramadhan Ali

Mhariri. Mohammed Abdulrahman