1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la Bajeti laitia mashakani serikali ya Kansela Scholz

Saumu Mwasimba
8 Desemba 2023

Kambi ya upinzani ya CDU/CSU yaishinikiza serikali ya Kansela Scholz kulipeleka bungeni suala la bajeti ya 2024 kupigiwa kura ya imani

https://p.dw.com/p/4Zuwg
Deutschland, Berlin | Olaf Scholz, Robert Habeck und ChristianLindner
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kambi ya upinzani nchini Ujerumani ya vyama ndugu  vya kihafidhina inazidi kuishinikiza serikali ya muungano inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz,kuhusiana na mgogoro wa bajeti.Chama cha Christian Democratic Union kimemtaka Scholz aitishe kura ya imani bungeni.Tamko la CDU limekuja baada ya hivi karibuni chama ndugu cha CSU nacho kutowa mwito wa kutaka uchaguzi wa mapema uitishwe.

Tamko la chama cha CDU linalomtia kishindo Kansela Scholz kuitisha kura ya imani kuhusiana na mgogoro wa bajeti na namna serikali yake inavyolishughulikia suala hilo,mara hii limetowa kwa katibu mkuu wa chama hicho  Carsten Linnemann ambaye jana akizungumza na kituo cha televisheni cha utangazaji cha umma ZDF alisema anafikiri itakuwa bora zaidi ikiwa Kansela atalifikisha bungeni suala hili kupigiwa kura ya imani.

Jengo la wizara ya fedha mjini Berlin
Jengo la wizara ya fedha nchini UjerumaniPicha: Hannes P. Albert/dpa/picture alliance

Kauli hii ya mwanasiasa huyo wa nafasi ya juu katika chama cha CDU imekuja baada ya siku ya Jumatano washirika wa serikali ya muungano kusema kwamba wataongeza juhudi  kutafuta namna ya kuziba pengo la Euro bilioni 17 katika bajeti ya mwaka ujao baada ya kushindwa kuutatua mgogoro huo wa bajeti katika mazungumzo ya usiku kucha,hali ambayo imezidisha wasiwasi kuhusiana na mipango ya nchi hii kubwa kiuchumi barani Ulaya.

Jana alhamisi mbunge mwandamizi kutoka chama cha Social Democratic SPD cha Kansela Scholz aliandika ujumbe mfupi wa simu ulioonekana na shirika la habari la Ujerumani Dpa akisema kwamba bunge halitokuwa na muda mwaka huu wa kupiga kura juu ya bajeti ya mwaka ujao.

Katja Mast kwenye ujumbe wake aliweka wazi kwamba ingawa wamefanya juhudi zote kwa uwezo wao,suala hilo la bajeti ya mwaka 2024 haliwezi tena kukamilishwa mwaka huu kwa muda unaotakiwa.Kwa  upande mwingine katibu mkuu wa chama hicho cha SPD Kevin Kühnert alisema katika mpango huu wa bajeti ana uhakika kwamba Scholz anaungwa mkono na pande zote za serikali ya mseto.

Kansela Olaf Scholz akijadili suala la bajeti na viongozi wa serikali yake
Kansela Olaf Scholz na waziri wa uchumi Robert Habeck pamoja na waziri wa fedha Christian Lindner,wakiwa kwenye majadiliano ya serikaliPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Soma pia: Rungu la Mahakama latikisa sehemu ya bajeti ya UjerumaniSerikali hiyo inayoundwa na vyama vya Social Democratic,SPD,Kijani na Waliberali -Free Democratic,FDP iko kwenye shinikizo kubwa ikitakiwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa bajeti uliosababishwa na uamuzi wa kihistoria wa mahakama uliozima mipango ya serikali hiyo ya kutaka kutumia fedha zilizobakia katika fungu na kupambana na ugonjwa wa Uviko 19,katika kusimamia miradi ya mazingira.

Mpaka sasa chama cha FDP kinachowapendelea zaidi wafanyabiashara kimeondowa uwezekano wa kukubaliana na suala la kuongezwa kodi au kuchukua mkopo wakati vyama vya SPD na kijani wakipinga kupunguzwa kwa matumizi ya maeneo kama  ustawi wa jamii.

Bunge la Ujerumani
Bunge la UjerumaniPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Katibu mkuu wa chama cha upinzani CDU, Carsten Linnemann amesema ikiwa Kansela Scholz atashinda kura ya imani bungeni serikali ya mseto italazimika kuandaa mpango wa miaka mingine miwili ijayo na ikiwa itashindwa kwenye kura hiyo ya imani basi wananchi watabidi waamue juu ya mwelekeo mpya wa taifa.

Mwanasiasa huyo ambaye ndiye wa hivi karibuni kabisa kuongeza shinikizo dhidi ya serikali kuu amesisitiza kwamba sasa wanataka uwazi na ukweli na kwamba nchi hii haiwezi kuvumilia kwenda kama ilivyo sasa kwa miaka mingine miwili ijayo.Kwa upande mwingine katika barua iliyoandikwa na katibu wa bunge wa kundi la wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU,Thorsten Frei amemtaka spika wa bunge Bärbel Bas,kuingilia kati suala hili.