1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Subira ya Uturuki yayoma

Mohamed Dahman25 Oktoba 2007

Rais Abdullah Gul wa Uturuki amewaonya waasi wa Kikurdi leo hii kwamba subira ya Uturuki inafikia kikomo baada ya vilkosi vya Uturuki kusema kwamba wamezima shambulio la waasi hao karibu na mpaka wa Iraq.

https://p.dw.com/p/C77V
Rais Abdulla Gul wa Uturuki awaonya waasi wa Kikurdi.
Rais Abdulla Gul wa Uturuki awaonya waasi wa Kikurdi.Picha: AP

Serikali ya Uturuki imewaweka wanajeshi wake 100,000 kwenye mpaka wake wa milima kwa uwezekano wa kuvuka mpaka huo kwa ajili ya operesheni ya kuwatokomeza waassi takriban 3,000 wa chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi cha PKK ambao huishambulia Uturuki kutoka eneo la kaskazini mwa Iraq.

Wanadiplomasia wa Iraq,Uturuki na Marekani wameongeza juhudi zao za kuepusha operesheni hiyo kubwa ya kijeshi ya Uturuki ndani ya Iraq lakini Gul amesema Uturuki ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Kujihami Mataifa ya Magharibi NATO haitovumilia tena mashambulizi zaidi ya PKK kutoka Iraq.

Gul ameuambia mkutano wa uchumi mjini Ankara kwamba wameazimia kabisa kuchukuwa hatua zote zinazohitajika kukomesha tishio hilo na kwamba Iraq haipaswi kuwa chanzo cha tishio kwa majirani zake.

Amekaririwa akisema kwamba juu ya kuwa wanaheshimu haki ya kujitawala na umoja wa Iraq subira ya Uturuki imekuwa ikielekea ukingoni na hawatovumilia utumiaji wa ardhi ya Iraq kwa harakati za kigaidi.

Marekani imekuwa mbioni kuepeusha shambulio kubwa la Uturuki kaskazini mwa Iraq kwa kuhofia kwamba litadhoofisha sio tu eneo lenye amani kabisa nchini humo bali pia eneo zima la Mashariki ya Kati.

Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amewaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini Romania kwamba Marekani yumkini ikawa haiwataki wafanye operesheni kubwa ya kijeshi lakini ni wao ndio watakaoamuwa kufanya operesheni hiyo au la.

Shinikizo la wananchi kwa serikali ya Uturuki kuchukuwa hatua linazidi kupamba moto tokea waasi wa Kikurdi kuwauwa wanajeshi 12 mwishoni mwa juma lililopita.Chama cha PKK ambacho kimetajwa na Marekani,Uturuki na Umoja wa Ulaya kuwa ni chama cha kigaidi kimesema kimewateka wanajeshi wanane wa Uturuki.

Duru za usalama za Uturuki zimethibitisha kuingia kwa ndege zao za kivita na majeshi ya ardhini mara kadhaa kwenye ardhi ya Iraq tokea Jumapili juu ya kwamba serikali ya Uturuki bado inataraji kwamba diplomasia inaweza kuepusha haja ya kuvamiwa kwa eneo hilo la kaskazini mwa Iraq.

Maafisa wa usalama wa nchi hiyo wameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba vifaru vya Uturuki na mizinga vimesaidia kuzima shambulio la waasi 40 wa PKK hapo jana usiku katika kituo cha kijeshi kwenye jimbo la Hakkari karibu na mpaka.

Kufuatia mapigano makali waasi hao wa Kikurdi walirudi kaskazini mwa Iraq wakiwa na wenzao kadhaa waliouwawa na waliojeruhiwa.

Ndege aina ya F-16 zimeruka mapema leo hii kutoka uwanja wa ndege wa Diyarbakir mji mkubwa kabisa wa mkoa wa kusini mwa Uturuki unaokaliwa na Wakurdi wengi.Haijulikani ndege hizo zimelekea wapi.

Katika ziara inayoelezewa na maafisa wa serikali ya Uturuki kuwa ni fursa ya mwisho kwa juhudi za kidiplomasia ujumbe unaoongozwa na waziri wa ulinzi Generali Abdel Qader Jassim ukijumuisha wajumbe wa serikali ya Kikurdi ya kaskazini mwa Iraq unatarajiwa kuwasili mjini Ankara baadae leo hii.

Wakati huo huo Marekani imesema serikali ya Iraq inapaswa kuchukuwa hatua kuwakamata wapiganaji wa Kikurdi wakati wakitoka kwenye maficho yao milimani na kuzuwiya kupeleka silaha kwenye kambi za waasi.