1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan kukumbwa na hali ngumu mwaka huu

Josephat Nyiro Charo11 Machi 2010

Shirika la wakimbizi la Norway laonya kuhusu kutokea mapigano

https://p.dw.com/p/MQa4
Kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit (kushoto) na rais wa Sudan Omar al-BashirPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Ripoti ya shirika la kutoa misaada la Norway inasema kwamba Sudan kusini, ambayo haijajitawala, itakumbwa na hali ngumu mwaka huu itakayodumazwa na mapigano ya kikabila na njaa. Haya yametabiriwa huku Sudan ikijiandaa kwa uchaguzi wa vyama vingi mwezi Aprili kama ilivyoafikiwa katika makubaliano ya amani ya mwaka 2005.

Baada ya kuchelewa mara nyingi, Sudan itafanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwezi Aprili mwaka huu. Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza katika kipindi cha miaka 24 na ni kipengee muhimu kwenye mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza vita vya zaidi ya miaka 20 kati ya eneo la kaskazini na kusini. Januari 9 mwakani, Sudan Kusini itafanya kura ya maoni ambayo wachambuzi wengi wanaamini itasababisha kuundwa nchi mpya barani Afrika.

Baraza la wakimbizi la Norway limesema jumuiya ya kimataifa lazima ihakikishe mkataba wa amani kati ya kaskazini na kusini unatekelezwa ipasavyo na pia usaidie kuboresha hali ya kimaisha katika Sudan Kusini na uepushe umwagaji damu ikiwa itakuwa nchi huru.

Ripoti hiyo ya shirika la kutoa misaada la Norway inasema misaada na visa vya raia kupoteza makaazi yao vitaendelea mwaka huu kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Ripoti hiyo inaongeza kusema kwamba mikakati ya kushughulikia mikasa ya dharura inafaa kuimarishwa hasa ikizingatiwa kwamba mapigano ya kusini mwa Sudan yanasababishwa na ukosefu wa chakula na pia maeneo ya kihistoria yanayoweza kuchochea tena mapigano kati ya kaskazini na kusini.

Hatua za kutekeleza mkataba wa amani wa mwaka wa 2005 imekuwa ya polepole na kaskazini imelaumiwa kwa kukosa msukumo wa kisiasa wa kutekeleza majukumu yake na kusini haina uwezo wa kimsingi kuyaafikia.

Ripoti hiyo ya shirika la misaada la Norway pia inadokeza kwamba ukosefu wa makubaliano kuhusu masuala tete ikiwemo kucheleweshwa kwa kuweka mpaka kati ya kaskazini na kusini na jinsi mapato ya mafuta yatakavyogawanywa baada ya kura ya maoni kunaweza kusababisha vita vipya.

Ripoti hiyo inapendekeza kwamba ikiwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe hayatasuluhishwa kusini mwa Sudan, basi huenda mkataba wa amani wa mwaka wa 2005 ukakosa maana hasa mahitaji ya msaada ya kusini yakitiliwa maanani.

Wachunguzi wanasema kwamba kiasi cha watu 2500 walifariki mwaka jana katika mapigano ya kusini baina ya wafugaji wa makabila tofauti ambayo historia yao ilighubikwa na vita iliyochangia jamii nyingi kutumia silaha.

Mwaka wa 2008, raia 187,000 walipoteza makaazi yao na wengine takriban laki nne walitoroka kutokana na kutchacha kwa mapigano yaliyochangiwa na ukosefu wa chakula na kupuuzwa kisiasa kwa jamii za wachache wa kusini.

Ripoti hiyo maarufu kama NRC inasema kwamba asilimia 80 ya huduma za afya na elimu kusini mwa Sudan hutolewa na mashirika ya misaada na hayawezi kumudu kwa muda mrefu.

Kiasi cha raia milioni mbili waliuawa na wengine milioni nne kuachwa bila makaazi katika vita kati ya kaskazini na kusini, vita vibaya zaidi katika historia ya bara la Afrika. Amani kati ya kusini na kaskazini ni muhimu kwa amani na maendeleo ya kiuchumi katika kanda ya Afrika Mashariki.

Mwandishi: Peter Moss/ Reuters

Mhariri: Josephat Charo