1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini: Watu 50 wauawa Juba kufuatia mzozo wa mifugo

29 Novemba 2017

Watu 50 wameuawa katika mzozo wa kugombea mifugo katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini, miongoni mwao wakiwemo watoto saba. Wizi wa mifugo umekuwa ukifanyika kwa karne kadhaa Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/2oTJw
Südsudan Bewaffneter Hirte 23.12.2013
Picha: Reuters

Watu 50 wameuawa katika mzozo wa kugombea mifugo katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini, miongoni mwao wakiwemo watoto saba. Waziri wa habari wa jimbo hilo, Akech Dengdit amesema wanawake 23 na wanaume 10 pia waliuawa jana asubuhi katika kile alichosema ni shambulizi la pamoja lililosababishwa na wezi wa mifugo na waasi wanaomtii Riek Machar.

Ameitaka serikali kuu ya Sudan Kusini kupeleka jeshi na polisi katika maeneo ya ndani kwenye jimbo la Jonglei ili kuimarisha usalama na kupambana na ghasia na wizi wa mifugo.

Wizi wa mifugo umekuwa ukifanyika kwa karne kadhaa Sudan Kusini na mara nyingine watoto wanatekwa nyara wakati wa wizi huo ili wafanye kazi za utumwa majumbani. Nchi hiyo pia iko katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo maelfu ya watu wameuawa tangu mwaka 2013 baada ya kutokea mpasuko kati ya Rais Salva Kiir na Machar, aliyekuwa makamu wa rais.