1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yapinga pendekezo la wanajeshi zaidi

Admin.WagnerD12 Agosti 2016

Mapigano makali mjini Juba, Sudan Kusini yalioshuhudiwa tangu mwezi jana yameibua hofu ya kuzuka upya kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwezi Agosti mwaka 2015 .

https://p.dw.com/p/1JfrO
China UN-Friedenstruppen für Südsudan
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa Wajiandaa kuelekea Sudan KusiniPicha: picture-alliance/dpa/C. Boyuan

Sudan Kusini hapo jana ilipinga pendekezo la Marekani kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka wanajeshi elfu 4 zaidi nchini humo kusaidia katika udumishaji amani na kusema hatua hiyo itahujumu uhuru wa nchi hiyo na kutishia kuirejesha nchi hiyo katika enzi za ukoloni.

Mwezi uliopita, serikali hiyo ilisema kuwa itaruhusu kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi mjini Juba baada ya mapigano kati ya majeshi ya Rais Salva kiir na wanajeshi wanaomuunga mkono mpinzani wake aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar kusababisha vifo vya mamia ya watu mjini humo.

Matakwa ya Sudan Kusini

Lakini hapo jana waziri wa habari wa Sudan Kusini Michael Makuei alisema kuwa jeshi hilo linapaswa kuwa huru badala ya chini ya amri ya Umoja wa Mataifa. Makuei alisema kuwa hatua ya Marekani ya kuilazimu nchi hiyo kukubali wanajeshi hao zaidi ni hatua ya kibeberu.

Chini ya pendekezo hilo la Marekani, wanajeshi hao wa ziada watakuwa chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS,lililo na wanajeshi takriban elfu 12.

Südsudan UN denken über Verstärkung von Unmiss nach
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wathibiti raia Sudan Kusini kabla kusambaza chakula cha msaada.Picha: Reuters/A. Ohanesian

Shutuma za Sudan Kusini

Sudan Kusini imeishutumu UNMISS kwa kushindwa kuwalinda raia wa nchi hiyo. Kulingana na balozi wa Marekani nchini Sudan Kusini, Molly Phee, pendekezo hilo la Marekani linaambatana na matakwa ya jumuiya ya ushirikiano wa kimaendeleo wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD na Sudan Kusini ni mwanachama wa IGAD.

Baraza la usalama litapiga kura hapo kesho kuhusu pendekezo hilo la iwapo kutumwe wanajeshi zaidi Sudan Kusini au la. Hayo yajiri huku Umoja wa Mataifa ukisema takriban raia 70,000 wa Sudan Kusini walilazimika kutorokea nchi jirani ya Uganda baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo mwezi uliopita.

Mwandishi. Tatu Karema, AFPE; AP

Mhariri: Caro Robi