1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yatimiza mwaka mmoja wa uhuru

9 Julai 2012

Umetimia mwaka mmoja tangu Sudan Kusini ijitangaze kuwa taifa huru. Kuanzia saa sita za usiku, raia wa nchi hiyo wamekuwa wakisherehekea katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.

https://p.dw.com/p/15Twx
Bendera ya Sudan Kusini
Bendera ya Sudan KusiniPicha: Reuters

Shamrashamra za maadhimisho ya mwaka mmoja wa uhuru zilianzia leo usiku katika mji wa Juba. Watu walikuwa wakiimba na kucheza katika mitaa ya mji huo huku wengine wakipiga honi za magari yao kwa sauti kubwa kufurahia siku hii muhimu kwa taifa lao. "Leo ni siku nzuri kwa sababu ni sikukuu ya kuzaliwa kwa nchi yangu," alisema Rachel Adau, ambaye amehudhuria sherehe rasmi za kuadhimisha Uhuru wa Sudan Kusini, katika uwanja ulio karibu na kaburi la kiongozi wa zamani wa waasi, John Garang.

Miongoni mwa watu wanaohudhuria sherehe hizo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Jean Ping pamoja na rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, anayeongoza mazungumzo ya kuleta amani baina ya Sudan na Sudan Kusini. Viongozi kutoka Ethiopia, Kenya na Uganda pia wanahudhuria sherehe hizo.

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping
Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean PingPicha: Reuters

Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya sherehe za leo, hakuna viongozi wa juu kutoka Sudan wanaoshiriki katika sherehe hizo. Hali ilikuwa tofauti mwaka mmoja uliopita, ambapo Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo alialikwa katika hafla ya kusherehekea uhuru wa Sudan Kusini.

Miundombinu bado yahitajika

Uhuru wa nchi hiyo unachukuliwa kuwa hatua ya muhimu ya kisiasa. Lakini katika masuala ya kiuchumi, taifa hilo bado halijapiga hatua. Licha ya kwamba Sudan Kusini ina utajiri mkubwa wa mafuta, miundombinu kama vile barabara, shule, hospitali pamoja na huduma ya maji safi na umeme bado ni duni sana.

Sherehe za uhuru mwaka jana
Sherehe za uhuru mwaka janaPicha: dapd

Hata hivyo, Profeesor Abraham Matoc Dhal wa chuo kikuu cha Rumbek kilichopo Sudan Kusini inaeleza kwamaba hatua za maendeleo zimeshapigwa hasa katika mji mkuu Juba. "Unapofika katika mji mkuu Juba, unaona tofauti. Kuna barabara mpya ambazo hazikuwepo kabla ya uhuru, majengo ya wizara yaliyofyniwa ukarabati na vile vile ujenzi unaoendelea kwa kasi. licha ya matatizo mengi yaliyopo, hali yamaisha imeboreshwa," alieleza Dhal.

Mafuta ndio chanzo kikuu cha mapato

Tatizo kubwa linaloikumba Sudan Kusini ni kwamba haiwezi kuuza mafuta yake nje ya nchi bila ya kutumia mabomba ya kupitishia mafuta hayo yanayopita katika eneo la Sudan. Tangu kujitenga kwa Sudan Kusini, mataifa hayo mawili yameshindwa kuafikiana juu ya malipo ya kupitisha mafuta katika mabomba. Serikali ya Sudan inataka ilipwe dola za Kimarekani 36 kwa kila pipa moja la mafuta litakalopitishwa, lakini serikali ya Sudan Kusini iko tayari kulipa dola moja tu kwa pipa.

Sudan na Sudan Kusini zimekuwa katika mgogoro wa mafuta
Sudan na Sudan Kusini zimekuwa katika mgogoro wa mafutaPicha: AP

Mwanzoni mwa mwaka huu, Sudan Kusini iliishutumu Sudan kwa wizi wa mafuta na tangu wakati huo ikasimamisha uchimbaji wa mafuta. Uamuzi huo umeifanya akiba ya fedha kwenye hazina ya nchi hiyo imalizike kabisa, kwani mauzo ya mafuta yanaingiza asilimia 90 ya mapato yake.

Mwandishi: Lina Hoffmann/Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Mohammed Khelef