1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan na JEM -maafikiano ya Dafur

24 Februari 2010

Emir wa Qatar na mfuko wa dala bilioni 1 kwa Dafur

https://p.dw.com/p/M9lS
Omar al-Bashir wa SudanPicha: picture alliance / abaca

SUDAN NA JEM

Sudan na kundi kubwa kabisa la waasi wa jimbo la Dafur,(JEM), zimetiliiana saini hapo jana usiku mjini Doha,mapatano ya kusimamisha vita na ya mfumo wa kufikiwa muwafaka wa mwisho juu ya amani nchini Sudan.Mapatano hayo yanahitaji hatahivyo, pia kuungwamkono na vikundi vyengine vya waasi wa Dafur. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameyaeleza mapatano hayo " ni hatua muhimu" kuelekea amani.Nae Emir wa Qatar, ametangaza mfuko wa dala bilioni 1 kuijenga upya Dafur.

MAPATANO:

Makubaliano hayo ya muda, yanaingiza mambo 12; na yanalipa kundi la waasi la "Justice and Equality Movement "(JEM) kwa ufupi, kundi kubwa kati ya yote ya waasi, nafasi ya kugawana madaraka nchini Sudan ambako uchaguzi wa rais na wa Bunge, umepangwa kufanyika hapo April.Mapatano ya Doha yalitiwa saini na rais Omar al-Bashir wa Sudan na Kiongozi wa JEM ,Khalil Ibrahim mbele ya Emir wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani pamoja na Rais Idriss Deby wa Jamhuri ya Chad na rais Issias Afeworki wa Eritrea.

Kiongozi wa JEM, alitumai kwamba, vikundi vyengine vya waasi wa Dafur,vingejiunga makubaliano hayo kwa masilhai ya umma wa Dafur.Mshauri wa rais Al-Bashir wa sudan kwa mkoa wa Dafur,Ghazi Salaheddine alietia saini ya kwanza ya mapatano haya hapo jumamosi,ameelezea matumaini pia kwamba vikundi vyengine vya waasi wa Dafur vitajiunga na mazungumzo na serikali ya Khartoum.

Kifungu cha 3 cha mapatano kinasema kuwa, serikali ya Sudan na kundi la JEM, zinaafikiana kushirikishwa kwa JEM katika hadhi zote za mamlaka nchini Sudan.Pande hizo mbili halkadhalika, zimekubaliana kwamba, JEM itageuka chama cha kisiasa mara tu mapatano ya mwisho ya amani yametiwa saini kati ya pande hizo mbili hadi ifikapo machi 15 mwaka huu.

MAONI JUU YA MAPATANO

Utiaji saini mapatano ya jana huko Doha, ulicheleweshwa kwa zaidi ya masaa 2 baada ya JEM,kuitaka serikali ya Sudan, kuridhia kuahirisha uchaguzi mkuu uliopangwa mwezi ujao,lakini, maafikiano juu ya hili hayakufikiwa.

Katibu mkuu wa UM Ban Ki -moon, ameyakaribisha mapatano ya Doha na kuyaeleza ni "hatua muhimu".Marekani nayo imeyapongeza mapatano ya Doha na kuyaita "hatua muhimu" kuelekea mazungumzo rasmi yatakayo rejewa baadae huko Qatar.Uingereza pia imeyasifu mapatano huku waziri wake anaehusika na maswali ya Afrika, Gleny Kinnock, akisema pande zote nchini Sudan, zinapaswa sasa kuongeza mara mbili juhudi zao kufikia amani.

MFUKO WA DALA BILIONI 1

Emir wa Qatar, ametangaza mfuko wa dala bilioni 1 kuichangia Dafur kujengwa upya .Rais Omar al-Bashir, alisema kabla ya kutiwa saini mapatano haya kwamba, mwaka huu utajionea kuzaliwa kwa "Sudan mpya" yenye amani, utulivu na ilioungana kutokana na nia ya wananchi wake.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman