1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan ya Kusini yaamua kuwa huru?

17 Januari 2011

Hata kabla ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa rasmi, waangalizi wa kimataifa tayari wameshaidhinisha kuwa watu wa Sudan ya Kusini wameamua kujitenga na Kaskazini na kuwa taifa jipya huru duniani.

https://p.dw.com/p/zytT
Wasudan ya Kusini kwenye kura ya maoni
Wasudan ya Kusini kwenye kura ya maoniPicha: picture alliance/dpa

Matokeo ya mwanzo ya zoezi hilo la kura ya maoni iliyofanyika wiki iliyopita yameshaonyesha kwamba watu wa jimbo la Sudan Kusini lenye utajiri mkubwa wa mafuta wameamua kujitenga na upande wa Kaskazini na kuwa taifa huru,baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wasimamizi wa kimataifa kama kutoka kituo cha Carter pamoja na Umoja wa Ulaya wamelisifu zoezi la kura ya maoni kwa kusema limefanyika vizuri na kwa njia ya haki jambo ambalo limetoa moja kwa moja msimamo wa kimataifa wa kuidhinisha matokeo ambayo yamelisogeza jimbo hilo hatua moja mbele kuelekea uhuru wake kamili wa kujitawala.

Wapiga kura wa Sudan ya Kusini
Wapiga kura wa Sudan ya KusiniPicha: AP

Ujumbe wa rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter ulidokeza kwamba pamoja na kujitokeza kwa dosari ndogondogo lakini hazikuharibu wala kusababisha kura hiyo kutokuwa halali na bila shaka kujitenga kwa Sudan kunatarajiwa kumaliza mzizi wa fitna unaosababisha mvutano mara nyingi kati ya watu wa Kaskazini na Kusini.

Taarifa ya wakfu wa Carter iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kwamba hatua nzima ya kura ya maoni hadi kufikia hivi sasa imekwenda chini ya viwango vya kimataifa na inaweza kutajwa kwamba imefanyika kwa njia ya kidemokrasia na kuwakilisha maoni halisi na nia ya wakaazi wa Sudan Kusini.

Chama tawala cha Sudan Kusini kimewapongeza wasimamizi kutoka nje pamoja na jinsi walivyotathmini zoezi hilo kwamba limefanyika kwa njia ya kidemokrasia lakini chama hicho kimekataa kutangaza ushindi,badala yake kimesema hilo litafanyika wakati matokeo rasmi yametangazwa.Hata hivyo matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu wa Januari wakati matokeo ya mwisho yakitegemewa kutangazwa Februari 14.

Itakumbukwa kwamba ujumbe wa wasimamizi kutoka nje ulijumuisha nchi sita za jumuiya ya Afrika Mashariki iliyodhamini mazungumzo yaliyochangia kupatikana makubaliano ya amani ya mwaka 2005. Kwa upande mwingine tathmini iliyotolewa na wasimamizi wa kimataifa katika zoezi hili imetofautiana kwa kiasi kikubwa na ile iliyotolewa na wasimamizi hao katika uchaguzi mkuu wa Sudan nzima mwezi Aprili mwaka jana ambapo waasi wa zamani walinyakua asilimia 93 ya kura katika jimbo hilo la Kusini.

Wakati huohuo kiongozi wa chama cha upinzani cha Kiislamu, Hassan al-Turabi, amesema kwamba mtindo wa vuguvugu lililotokea huko Tunisia unaweza pia kushuhudiwa Sudan Kaskazini kufuatia malalamiko ya hali ya uchumi yanayozidi kupata makali pamoja na hofu ya kujitenga kwa Kusini. Itakumbukwa kwamba Sudan imeshawahi kukumbwa mara mbili na vuguvugu za kisiasa na kuangushwa kwa tawala za kijeshi katika miaka ya 1964 na 1985.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFPE/Reuters

Mhariri: Mohammed AbdulRahman.