1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan zatakiwa kurejea katika meza ya mazungumzo

18 Mei 2012

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka Sudankufikia makubaliano juu ya eneo lenye mafuta la Abyei. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeongeza muda wa kuwepo kwa vikosi vya usalama vya umoja huo kwa miezi sita.

https://p.dw.com/p/14xNS
Eneo la Abyei lenye mafuta
Eneo la Abyei lenye mafutaPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza kuwa hali iliyopo sasa katika eneo la mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini ni tishio kwa usalama na limepitisha azimio la kudai pawepo na utawala wa pamoja na kikosi cha polisi kitakachoendeshwa na nchi zote mbili. Baraza la Usalama limeitaka pia Sudan iondoe mara moja wanajeshi wote kutoka Abyei, kufuatia Sudan Kusini kuwaondoa maafisa wa polisi wapatao 700 wiki iliyopita.

Baraza la Usalama lilitishia kuziwekea vikwazo visivyo vya kijeshi Sudan na Sudan Kusini iwapo nchi hizo hazitosimamisha mapigano na kurejea katika meza ya mazungumzo. Mazungumzo ya kuleta amani yalikwama baada ya Sudan Kusini kuliteka eneo lenye utajiri wa mafuta la Heglig, ambalo sasa limechukuliwa tena na Sudan.

Uchimbaji wa mafuta katika eneo la Heglig
Uchimbaji wa mafuta katika eneo la HegligPicha: Reuters

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilichopo katika eneo la Abyei kinajumuisha askari wapatao 4,000. Kikosi hicho kilitumwa baada ya Sudan kuliteka eneo la Abyei mwaka jana, kabla ya Sudan Kusini kujitangazia uhuru wake.

Mbeki afanya mazungumzo na Sudan mbili

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye ni mjumbe wa kuleta amani kati ya Sudan na Sudan Kusini, jana jioni aliwasili katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Mbeki pamoja na wanadiplomasia wengine wanajaribu kuyaanzisha tena mazungumzo ya kuleta amani kati ya Sudan mbili. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Sudan, Al-Obeid Meruh, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Mbeki katika ziara yake ya siku mbili atakutana na rais Omar Hassan al-Bashar wa Sudan na anatarajiwa pia kuutembelea mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo MbekiPicha: AP

Akizungumza na Deutsche Welle, aliyekuwa kiongozi wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Peter Schumann alisema: "Nina mashaka kwamba Bwana Mbeki hatofanikiwa katika mazungumzo yatakayofanyika Khartoum. Vile vile nina mashaka kuwa hatakuwa na mafanikio Juba kwani serikali ya Juba imeeleza wazi wazi kwamba matumaini yake juu ya mazungumzo ya kuleta amani yanayoongozwa na Bwana Mbeki yamefifia"

Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Bw. Barnaba Marial Benjamin, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wajumbe kutoka nchini kwake wako tayari kufanya mazungumzo na Thabo Mbeki lakini mpaka sasa, Mbeki hajawapa mwaliko rasmi.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/AP/AFP

Mhariri: Josephat Charo