1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sura za nchi zilizo mashuhuri kabisa barani Afrika hatarini kutoweka .

Mohmed Dahman11 Juni 2008

Baadhi ya sura za nchi zilizo mashuhuri kabisa Afrika kama vile Mlima Kilimanjaro ulio na barafu kileleni mwake na Ziwa Chad viko hatarini kutoweka milele ikiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani.

https://p.dw.com/p/EHWf
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa(UNEP) Achim Steiner.Picha: AP

Hayo ni kwa mujibu wa repoti ya Umoja wa Mataifa inayoelezea juu ya sehemu za alama mashuhuri za Afrika zilioko katika hatari ya kutoweka katika ramani ya dunia.

Akizinduwa kitabu cha ramani mpya ya bara la Afrika mjini Johannesburg Afrika Kusini ramani ambayo inaonyesha kubadilika kwa haraka sana kwa maumbile yake ya asili mkuu wa shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP amesema ni muhimu kwamba jumuiya ya kimataifa inafikia makubaliano mapya juu ya mabadiliko ya hali ya hewa kabla ya mkutano wa dunia uliopangwa kufanyika mjini Copenhagen Danmark mwakani.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la mazingira la Umoja wa Mataifa Achin Steiner amewaambia waandishi wa habari kwamba wanahitaji ufumbuzi ambao sio tu utapunguza kwa kiasi kikubwa sana utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira duniani bali pia utaharakisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya marekebisho ya kuendana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa na kujenga uchumi utakaohimili mabadiliko hayo ya hali ya hewa pamoja na kushughulikia tatizo la umaskini na kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milinia.

Kitabu hicho cha ramani kina picha za taswira mbali mbali za zaidi ya alama 100 mashuhuri za nchi zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka 35 iliopita.

Baadhi ya habari za kushtuwa za repoti hiyo zinajumuisha picha za satalaiti za barafu ya Mlima Kilimanjaro ambayo imekuwa ikitoweka tokea mwanzoni mwa karne ya 20.

Utafiti wa repoti hiyo unaonya kwamba Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania ambao ni mlima mrefu kabisa barani Afrika unaweza ukapoteza kabisa barafu yake ilioko kileleni ifikapo mwaka 2020. Pia imeelezea jinsi barafu katika Milima Rwenzori nchini Uganda ilivyopunguwa kwa asilimia 50 kati ya mwaka 1987 na mwaka 2003.

Ziwa Chad na Ziwa Viktoria ambavyo ni vyanzo viwili muhimu kabisa vya maji barani Afrika yote yameonyeshwa kuwa yanakauka.

Mimea ya aina yake kwenye mwambao wa Cape Town nchini Afrika Kusini ambayo majani yake huwa magumu na yenye ncha kama sindano pia imepunguzwa kwa kiasi kikubwa sana kutokana na kuendeleza miji katika kipindi cha miongo mitatu iliopita wakati kutanuliwa kwa miji mikuu kama vile Dakar wa Senegal kutoka maji ya bahari ya kiwango cha wastani kumesababisha taathira kubwa kwa mazingira.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliotolewa mjini Johannesburg Afrika Kusini kupotea kwa misitu ni tatizo kubwa katika nchi 35 ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Malawi,Nigeria na Rwanda miongoni mwa nchi nyengine.

Kitabu hicho cha ramani kinasema Afrika inapoteza zaidi ya hekta milioni nne pungufu kidogo ya maili mraba 15,000 za misitu kila mwaka kiwango ambacho ni mara mbili ya kiwango cha wastani cha ukataji wa misitu duniani.

Imeongeza kusema kwamba wakati huo huo baadhi ya maeneo barani kote Afrika inasemekana kupoteza zaidi ya tani 50 za udongo kwa hekta kila mwaka.

Utafiti huo unasema kwamba mmonyonko wa udongo na uharibifu unaosababishwa na kemikali na vitendo vya watu umedhoofisha takriban asilimia 65 ya mashamba ya Afrika.

Ziada ya hayo utafiti wa repoti hiyo umebaini kwamba kilimo cha ukataji miti na kuunguza moto miti kukiambatana na matukio ya mara kwa mara ya kupiga kwa umeme barani kote Afrika kunafikiriwa kuwa kunachangia kuzuka kwa moto wa misituni.