1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi kuzungumzia mzozo wa Rakhine

Lilian Mtono
13 Septemba 2017

Aung San Suu Kyi wiki ijayo atazungumzia mzozo wa jimbo la Rakhine, katika hotuba ya kwanza tangu kuuawa kwa mamia kwenye machafuko yaliyosababisha karibu Waislamu wa Rohingya 380,000 kukimbilia Bangladesh

https://p.dw.com/p/2juCX
Myanmar - Aung San Suu Kyi
Picha: Reuters/E. Su

Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi wiki ijayo anatarajiwa kuuzungumzia mzozo katika jimbo la Rakhine, katika hotuba yake ya kwanza tangu kuuawa kwa mamia ya watu kwenye machafuko ambayo yamesababisha karibu Waislamu wa Rohingya 380,000 kukimbilia Bangladesh na kuichafua sifa yake ya kuwa mtetezi wa wanyonge.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa serikali Zaw Htay amesema Suu Kyi atazungumzia "maridhiano na amani ya kitaifa" kwenye hotuba yake kupitia televisheni Septemba 19. Amesema, mshindi huyo wa tuzo ya Nobeli anayeandamwa na makundi ya watetezi wa haki za binaadamu kwa kushindwa kuuzungumzia na kuwalinda Warohingya walio wachache, hatahudhuria mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wiki ijayo ili kukabiliana na mzozo huo unaofukuta nchini mwake.

Machafuko hayo yamesababisha kuwa mzozo wa kibinaadamu kati ya pande zote za mpaka na kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Suu Kyi kulaani kampeni za kijeshi, ambazo Umoja wa Mataifa imezielezea kama zina viashiria vya mauaji ya kimbari.

Hatua kali zinazochukuliwa na jeshi la Myanmar zilizoanzishwa kujibu mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Rohingya mnamo Agosti 25, zimepelekea mamia kwa maelfu ya Warohingya kukimbilia Bangladesh, ambayo inajaribu kuhakikisha inatoa msaada kwa wakimbizi wenye mshituko na njaa. Kiasi asilimia 60 miongoni mwao ni watoto.

Rohingya Krise in Bangladesch
Asilimia 60 ya wakimbizi wa Rohingya walioingia Bangladesh ni watotoPicha: DW/M.M. Rahman

Wakimbizi wengine 9,000 kutoka Rohingya wameingia Bangladesh Jumatano hii, umesema Umoja wa Mataifa wakati ambapo mamlaka zilizungumzia ujenzi wa kambi mpya kwa ajili ya maelfu ya watu wanaoingia ambao hawana makazi.

George William Okoth-Obbo ni kamishna mkuu msaidizi wa operesheni katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, alinukuliwa akisema, " Tuna dharura, ndani ya dharura. Kuliweka hili kwa neno moja, kwa pamoja tunatakiwa kufanya wajibu wetu kwa kiasi kikubwa kuanzia chakula hadi malazi kwa maelfu ya watoto na kina mama na kuwarejeshea namna ya kuanza tena kupata mahitaji muhimu ya maisha. Kwa ujumla tunaunganisha wajibu wetu, ndio sababu tuko hapa na mwenzangu wa IOM."

Aidha, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo hii lilipanga kujadili mzozo wa wakimbizi katika kikao cha ndani, wakati China ikitarajiwa kuzuia jaribio lolote la lawama kwa mshirika wake huyo wa Kusinimashariki mwa Asia. Kabla ya mkutano huo washindi 12 wa tuzo ya Nobeli walisaini barua ya wazi ya kulitaka baraza hilo kungilia haraka kwa kutumia namna yoyote ile inayowezekana kumaliza mzozo na uhalifu dhidi ya ubinaadamu unaofanyika Rakhine.

Katika hatua nyingine, kundi la kigaidi la Al-Qaeda limetangaza kuanzisha vita vya jihad nchini Myanmar kufuatia mauaji ya mamia kwa maelfu ya Waislamu wa Rohingya ambao wanasema jeshi linachoma nyumba zao na kuwachinja raia.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa jana jioni, kiongozi wa kundi hilo lenye itikadi kali amewataka waislamu duniani kote kuungana kuwasaidia Waislamu wa Rohingya walioko Myanmar, ambao 30,000 miongoni mwao wamekimbilia Bangaldesh katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Makundi kadhaa yenye itikadi kali yameandamana kuwaunga mkono Warohingya tangu kuanza kwa machafuko hayo. Kundi la kuwatetea Waislamu la Indonesia's Islamic Defenders Front limesema kiasi ya Waislamu 1,000 tayari wamekwishasaini kuunga mkono vita hivyo vya jihad nchini Myanmar.

Mwandishi: Lilian Mtono/dpae/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga