1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Swing States"- Majimbo yanayoamua matokeo ya uchaguzi

M.Knigge - (P.Martin)27 Oktoba 2008

Kama watu milioni 220 wana haki ya kupiga kura Marekani. Wapiga kura hao wametawanyika katika majimbo 51 na kila kura ni muhimu.Lakini baadhi ya kura hizo zina umuhimu zaidi kwani huweza kuamua matokeo ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/FiP8
Democratic presidential candidate Sen. Barack Obama, D-Ill., left, and Republican candidate Sen. John McCain, R-Ariz., shake hands at the finish of a presidential debate at Hofstra University in Hempstead, N.Y., Wednesday, Oct. 15, 2008. (AP Photo/J. Scott Applewhite)
Seneta Barack Obama(shoto) anaegombea urais kwa tikti ya chama cha Demokratik na mshindani wake, Seneta John McCain wa chama cha Republikan.Picha: AP

Majimbo yenye kura kama hizo,hujulikana kama "Swing States" na katika kila uchaguzi huwepo kama majimbo sita ya aina hiyo.Tarehe 4 Novemba mamilioni ya Wamarekani watapiga kura kumchagua rais mpya.Lakini ni kura za majimbo machache tu ndio huenda zikaamua nani atakaehamia Ikulu ya Marekani:BaracK Obama au John McCain. Kwani anaetaka kuwa rais wa Marekani si lazima kujizolea sehemu kubwa ya kura zilizopigwa na wananchi.Kilicho muhimu zaidi ni kujisombea wajumbe kwa uwingi mkubwa katika Jopo la Wajumbe.Kimsingi jopo hilo huonyesha matokeo ya kila jimbo na ye yote atakaeshinda jimboni hupewa kura za wajumbe wote katika jimbo hilo,bila ya kujali kiwango cha ushindi wake.

Desturi,majimbo mengi huelemea zaidi upande wa chama kimoja na matokeo ya uchaguzi huweza kutabiriwa hata kabla ya uchaguzi kufanywa. Lakini mara nyingi ni majimbo machache yanayoamua matokeo ya uchaguzi.Hayo ni majimbo ambako kura huweza kwenda upande wo wote.

Kwa hivyo katika siku za mwisho za kampeni,wagombea wote hujitokeza zaidi katika majimbo kama hayo.Na safari hii majimbo matatu yanayopewa kipaumbele zaidi Florida,Ohio na Pennsylvania yaliyoamua matokeo ya uchaguzi uliopita.Tangu mwaka 1960 hakuna aliekuwa rais bila ya kujinyakulia ushindi katika angalao majimbo miwili kati ya majimbo hayo matatu.

Kwa mfano Wademokrats wengi wapo katika sehemu za miji,mashariki mwa Pennsylvania wakati maeneo ya shambani katikati ya jimbo hilo, yakidhibitiwa na wale wanaoelemea upande wa chama cha Republikan. Lakini vipi wafanya kazi wa viwanda vya vyuma na makaa watapiga kura, huenda ukaamua matoeko ya uchaguzi katika jimbo hilo.Kwani mwaka 2000 na 2004 chama cha Demokratik kilijinyakulia ushindi kwa uwingi mdogo mno katika jimbo hilo.

Hata huko Ohio hali si tofauti.Jimbo hilo ni muhimu sana kwa John McCain. kwani hakuna Mrepublikan alieshinda uchaguzi bila ya kujinyakulia ushindi huko.Na ikiwa McCain anataka kuingia Ikulu ya Marekani basi hana budi kushinda katika jimbo la Florida pia.

Baadhi ya wapiga kura katika majimbo mengine wanakerwa na ukweli kuwa mara kwa mara ni majimbo machache yanayoamua matokeo ya uchaguzi.Vile vile wanalalamika kuwa kura zao hazipewi uzito.Lakini hali hiyo haitobadilika iwapo sheria za uchaguzi za nchi hiyo hazitorekebishwa.