1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria hali bado ni tete

Halima Nyanza29 Agosti 2011

Viongozi wa nchi iliyokuwa mshirika wa karibu Syria, Uturuki, wameonesha kumtupa mkono Rais Bashar al Assad kutokana na kutokuwa na imani naye, wakati majeshi yake yakiendelea kuwashambulia raia.

https://p.dw.com/p/12PJo
Vifaru vya jeshi la Syria katika jimbo la HomsPicha: picture alliance/dpa

Shirika linalohusika na masuala ya Haki za binadamu la Syria lenye makazi yake nchini Uingereza, limesema majeshi ya Syria yameingia katika kijiji cha Hit, kilomita mbili kutoka katika mpaka wa nchi hiyo na Lebanon.

Kiongozi wa shirika hilo Rami Abdel-Rahman ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kulikuwa na mapigano makali asubuhi ya leo.

Mapigano hayo yameendelea hii leo nchini Syria, licha ya mapema mwezi huu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kusema kwamba Rais wa Syria Bashar al Assad alimwambia kwa njia ya simu kwamba amesimamisha operesheni za kijeshi dhidi ya wapinzani.

Wiki iliyopita Ban Ki Moon alisema kwamba Rais Assad ameshindwa kutimiza ahadi yake.

Wakati hali ikiwa hivyo, katika maeneo ya Syria yaliyo mpakani mwa Lebanon, wakazi wa maeneo ya mji wa Rastan ulioko katikati ya Syria wameukimbia mji huo leo, kutokana na kuhofiwa kushambuliwa, baada ya wanajeshi kuuzingira, huku kukisikika milio ya risasi.

Wanaharakati nchini humo wamesema watu wameondoka kutokana na hofu baada ya vikosi vya jeshi kuanza kusambazwa kusini mwa mji huo ulioko katika jimbo la Homs.

Mji wa Rastan umekuwa ni eneo lenye nguvu kwa wapinzani wanaoipinga serikali.

Nchini Uturuki nako, Rais wa nchi hiyo Abdullah Gul na Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan kwa pamoja wamekosoa vikali hatua hizo kali zinazochukuliwa na majeshi ya Syria dhidi ya wapinzani wa serikali ya nchi hiyo.

Wamemtaka Rais Assad kuachana na hatua hizo, dhidi ya waandamanaji, iwapo kama kweli anataka kuepukana na yale yaliyomkuta kiongozi wa Misri Hosni Mubarak na wa Libya Muammar Gaddafi.

Rais Gul amenukuliwa na magazeti ya nchi hiyo akisema kwamba imefika wakati sasa, wamekosa imani na Rais Assad.

Lakini kwa upande wake balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vital Churkin amelikosoa azimio lililowasilishwa na nchi za nne za Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Syria kwa kusema kuwa linapendelea.

Katika hatua nyingine katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu Nabil al-Arabi anatarajiwa kuanza ziara nchini Syria katika juhudi za kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo, lakini kwa sasa kwanza anasubiri kupata kibali kutoka serikali ya Syria.

Jumla ya watu 2,200 wanaripotiwa wameuawa tokea kuanza kwa machafuko nchini Syria, huku watu 12 wakiriporiwa kuuawa jana Jumapili.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuter,afp)

Mhariri: Abdul-Rahman