1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria imepewa siku tatu kudumisha amani nchini humo

17 Novemba 2011

Huku Syria ikipewa siku tatu kusitisha mapigano, utawala wake sasa umewataka wafuasi wake kutofanya mashambulizi katika balozi za kigeni nchini humo

https://p.dw.com/p/13CIY
Rais wa Syria Bashar Al AssadPicha: AP

Kulingana na vyombo vya habari nchini Syria, serikali itachukua hatua kali kwa wale watakaokiuka na kufanya uvamizi huo. Wafuasi walio watiifu kwa rais Bashar al-Assad leo walivamia balozi za Qatar, Morocco na umoja wa Falme za kiarabu kulaani uamuzi uliotolewa na jumuiya ya nchi za kiarabu ya kuiondoa kwa muda Syria katika jumuiya hiyo.

Uamuzi huo uliafikiwa baada ya Syria kutotimiza matakwa ya umoja huo ya kusitisha mapigano na kuweka amani ya kudumu.

Hata hivyo wizara ya ndani ya Syria imeonya itachukua hatua kali za kisheria ikijumuisha kufungwa na kuhukumiwa mahakamani kwa yeyote yule atakayejaribu kuvamia balozi za kigeni nchini humo. Ufaransa na Morocco tayari zimewaondoa balozi wao nchini Syria. Ufaransa imefunga afisi zake pamoja na taasisi zake za tamaduni baada ya ujumbe wake kushambuliwa hivi maajuzi.

´

Kabla ya mashambulizi ya hapo jana kwa balozi za kigeni, Syria ilikuwa imetoa ujumbe kwa jumuiya ya nchi za kiarabu kupitia naibu waziri wake wa nchi za kigeni Faisal Mikdad kuwa kamwe serikali hiyo haitaruhusu visa kama hivyo kwa ubalozi kutokea tena.

Kwa upande wake baraza la usalama la umoja wa mataifa lilitoa kauli yake ya kulaani visa vya mashambulizi katika balozi za kigeni.

Ägypten Kairo Arabische Liga Beratung über Syrien
Jumuiya ya nchi za kiarabuPicha: picture-alliance/dpa

Maandamano au mashambulizi ya hapo jana yalifanyika wakati jumuiya ya nchi za kiarabu ikitoa onyo kali kwa rais Bashar al Assad kuwa inampa siku tatu kutekeleza matakwa yao ya kusitisha mapigano na kudumisha amani nchini humo au kuwekewa vikwazo vya kiuchumi.

Umoja wa mataifa umesema tangu ghasia kuanza Syria mnamo machi 15 mwaka huu zaidi ya watu 3,500 wameuwawa.

Huku hayo yakiarifiwa China imeonesha wasiwasi wake juu ya hali ilivyo nchini Syria. China ni moja ya nchi ambayo inashinikizwa kuungana na jumuiya ya nchi za kiarabu katika mpango wake wa kusitisha mapigano na umwagikaji wa damu Syria, yalioanza miezi minane iliyopita ya kumtaka rais wake kuondoka madarakani.

Liu Weimin, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China amesema wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ilivyo sasa nchini Syria.

Mwandishi Amina Abubakar/DPAE/ AFPE/APE

Mhariri Josephat Charo