1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria kuhodhi mkutano wa mawaziri wa nje wa G8

10 Aprili 2013

Waasi wa Syria kukutana na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mawaziri wengine wa mambo ya nchi za nje wa Kundi la Mataifa Manane Tajiri Duniani G8 wanaokutana London leo Jumatano (10.11.2012).

https://p.dw.com/p/18D2m
Upinzani wa Syria.
Upinzani wa Syria.Picha: AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa waasi Ghassan Hitto na makamo rais wa Muungano wa Kitaifa wa Syria George Sabra na Soheir Atassi wanatarajiwa kushinikiza madai yao ya kupatiwa silaha ili kusaidia kumuangusha Rais Bashar al-Assad. Masuala juu ya hofu ya kutumiwa kwa silaha za nyuklia na Korea ya Kaskazini na mpango wa nuklea wa Iran pia yanatarajiwa kuhodhi agenda ya mkutano.

Mkutano huo wa wanadiplomasia waandamizi kutoka kundi la Mataifa Manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda pia utazungumzia suala la Myanmar,Somalia, usalama katika mtandao na kuzuwiya dhila za ngono katika maeneo ya vita.

Syria agenda kuu ya mkutano

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema agenda kuu itakuwa juu ya hali ya Syria ambapo itakuwa mada ya kwanza kujadiliwa.Hague amesema amezungumzia suala la kuwapatia silaha waasi na viongozi watatu wa upinzani wa Syria wanaoitembelea Uingereza.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague.Picha: AP

Amesema viongozi hao wataweza kukutana na baadhi ya mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la Mataifa Manane leo hii kabla ya mawaziri hao kukutana kwa chakula cha jioni na kufuatiwa na mazungumzo rasmi hapo kesho.

Muungano wa Upinzani wa Taifa wa Syria unatambuliwa na Marekani na mataifa mengine mengi ya magharibi na nchi za Kiarabu kuwa mwakilishi pekee wa wananchi wa Syria.

Alipoulizwa iwapo serikali ya Marekani itaongeza msaada wake kwa waasi wa Syria waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ni wajibu wa Ikulu ya Marekani kutowa taarifa zozote zile. Lakini Hague amesema Uingereza na Ufaransa zitaendelea kushinikiza kuondolewa kwa vikwazo vya silaha dhidi ya Syria ili waweze kuwapatia silaha waasi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.Picha: Paul J. Richards/AFP/Getty Images

Wakati hayo yakijiri kundi la Al Qaeda nchin Iraq limethibitisha hapo jana tuhuma zilizokuwepo kwa muda mrefu kwamba inawasaidia wapiganaji majihadi nchini Syria. Jeshi Huru la Syria ambalo ni kundi kuu la wapiganaji waasi limejitenganisha na majihadi na kusisitiza kwamba ushirika wake na kundi hilo kuu la wapiganaji wa upinzani ni katika mbinu tu na kwamba lengo lake ni kuwa na Syria ya demokrasia.

Mkuu wa Al Qaeda nchini Iraq Abu Bakr al-Baghdadi amesema kundi la Al- Nusra ni tawi la Taifa la Kiislamu la Iraq.

Kauli hiyo ya Baghdadi inakuja siku moja baada ya mtindo wa kujitowa muhanga kwa kujiripua unaotumiwa na Al- Nusra kuuwa watu 15 na kujeruhi wengine 146 katikati ya Damascus.

Ufaransa imesema hapo jana inataka kuwa na mazungumzo na washirika wake wa Ulaya na katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya iwapo kuliorodhesha kundi hilo la Al-Nusra kama kundi la kigaidi.

Kundi la waasi la Al Nusra nchini Syria.
Kundi la waasi la Al Nusra nchini Syria.Picha: picture-alliance/AP

Serikali ya Marekani tayari imeliorodhesha kundi hilo kuwa kundi la kigaidi hapo mwezi wa Disemba kutokana na kuwa na mahusiano ya karibu na wapiganaji wa Al Qaeda ambao waliongoza uasi dhidi ya vikosi vya Marekani nchini Iraq kabla ya kuondolewa hapo mwaka 2011.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza lenye kuunga mkono upinzani hapo jana limesema kikosi kimoja cha waasi wa kundi la Ahrar Suriya kimekuwa kikiwatesa na kuwatishia raia katika mji wa kaskazini wa Allepo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef