1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yataka utawala wa Assad usalie madarakani

28 Septemba 2015

Rais wa Iran Hassan Rouhani ameonya kuwa serikali ya Syria inapaswa kuruhusiwa kusalia madarakani ili kuwazuia wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS kulidhibiti taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1GeSy
Picha: picture alliance/dpa/Sana Handout

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Iran Hassan Rouhani amehoji kuwa kinachopaswa kupewa kipaumbele ni kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS nchini Syria na kisha baadaye mageuzi ya kisiasa huenda yakafuata.

Rouhani ameliambia kundi la wasomi na wanahabari mjini New York kuwa ili kuweza kufanikiwa katika vita dhidi ya ugaidi, serikali ya Syria haipaswi kudhoofishwa.

Kiongozi huyo wa Iran hakuzungumzia moja kwa moja hatma ya Rais wa Syria Bashar al Assad lakini ameeleza bayana kuwa ni muhimu kuwepo mabadiliko ya utawala baada wanamgambo wa IS kushindwa.

Juhudi za kidiplomasia zashika kasi

Matamshi ya Rouhani yanakuja huku kukiwa na juhudi kabambe za kidiplomasia kuhusu njia bora ya kuvikomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria ambavyo vimedumu kwa miaka minne na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 240,000 na mamilioni ya wengine kuachwa bila ya makaazi wakitorokea nchi jirani na za Ulaya kama wakimbizi.

Rais wa Iran Hassan Rouhani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa
Rais wa Iran Hassan Rouhani katika makao makuu ya Umoja wa MataifaPicha: Reuters/C. Allegri

Urusi pia inashirikiana na Iran kuuimarisha utawala wa Rais Assad baada ya kutuma ndege za kivita nchini humo kupambana dhidi ya IS. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameelezea wasiwasi wake kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuwa kampeni hiyo ya kijeshi iliyoanzishwa itampa nguvu Assad na kumfanya kuzidi kung'angania madaraka na hivyo kutatiza juhudi za kutafuta amani Syria.

Rais Wa Urusi Vladimir Putin amesema kwa sasa hana nia ya kuyatuma majeshi yake nchini Syria. Rouhani anatarajiwa kuzungumzia mzozo huo wa Syria katika hotuba yake kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo baada ya Rais wa Marekani Barack Obama na Rais Putin kuhutubia.

Viongozi hao wa dunia wanatarajia kuangazia pakubwa mzozo huo wa Syria mwaka mmoja baada ya Rais Obama kuanzisha kampeni ya mashambulizi ya angani Syria na Iraq kupambana na IS.

Licha ya mabilioni ya dola kutumika na mashambulizi chungu nzima ya angani, kampeni hiyo ya kijeshi haionekani kufanikiwa kukabiliana vilivyo na wanamgambo hao wenye itikadi kali wanaoyadhibiti maeneo makubwa nchini Syria na Iraq.

Huku Ufaransa ikianzisha mashambulizi ya angani hapo jana nchini Syria dhidi ya IS, shinikizo la kumtaka Rais Assad kuondoka madarakani linaonekana kupungua makali.

Je Assad atasalia madarakani?

Ujerumani imetoa wito kuundwe serikali ya mpito nchini Syria kama sehemu ya juhudi za kuvimaliza vita nchini humo huku nchi za Umoja wa Ulaya zikionekana kulegeza msimamo wao kuhusu kuondoka madarakani kwa Assad.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Getty Images/AFP/J. Samad

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema Assad hawezi kuwa sehemu ya mustakabali wa Syria lakini vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa huenda akatumia hotuba yake katika Umoja wa Mataifa kubadilisha msimamo wake kumhusu kiongozi huyo wa Syria.

Obama na Putin wamepangiwa kukutana hii leo baada ya hotuba zao lakini maafisa wa serikali zote mbili wametofautiana kuhusu ni kipi viongozi hao wawili watakijadili. Putin pia atakutana na Rouhani na Rais wa Cuba Raul Castro.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/ap

Mhariri: Daniel Gakuba