1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria miaka miwili vitani

Tsuma Carolyne15 Machi 2013

Leo ni miaka miwili tangu ghasia kuanza Syria huku rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad akikataa kuondoka madarakani na viongozi wa Umoja wa Ulaya wakitofautiana kuhusu njia za kukomesha umwagikaji damu.

https://p.dw.com/p/17yQS
Waasi nchini Syria vitani
Waasi nchini Syria vitaniPicha: Getty Images

Ghasia nchini Syria zilianza tarehe15 mwezi Machi mwaka 2011 wakati waandamanji walipomiminika katika barabara za miji kadhaa nchini humo wakitiwa nguvu na wimbi la uasi lililokuwa limeyagubika mataifa ya Kiarabu wakitaka mabadiliko ya utawala wa kidemokrasia nchini mwao.

Licha ya waandamanji hao kutokuwa na silaha na wengi wao wakiwa wanawake na watoto kuandamana kwa amani, jeshi la Assad lilitumia nguvu kupita kiasi dhidi yao na hivyo basi kuchochea uasi na hatimaye waandamanaji kuanza kuchukua silaha.

Miaka miwili baadaye, Syria imeharibiwa pakubwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya watu elfu sabini, mamilioni kukimbilia hifadhi katika mataifa jirani, mamilioni wengine wakiwa hawajulikani waliko ama kuachwa bila makaazi na kusababisha janga la kiuchumi na kibinadamau.

Rais wa Syria Bashar Al Assad
Rais wa Syria Bashar Al AssadPicha: picture alliance / AP Photo

Waasi wakosa kuzungumza kwa sauti moja

Waasi nchini humo wanadhibiti maeneo mengi lakini kumekuwa na hali ya vuta nikuvute miongoni mwa makundi ya Waislamu walio na misimamo ya kadri na walio na misimamo mikali jambo ambalo limezua hofu ya kushindwa kuzungumza kwa kauli moja.

Akiwa anatokea kwenye familia ambayo imekuwa madarakani kwa miaka 40, Assad alidhani ataweza kwa urahisi kuwakandamiza waandamanaji kama alivyofanya baba yake, Hafez Assad, mwaka 1982 alipoukandamiza uasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu katika eneo la Hama na kuwauwa watu kati ya elfu kumi na arobaini.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel - Brüssel
Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel - BrüsselPicha: Reuters

Hadi sasa, jeshi la nchi hiyo lina zana kali za kivita na hivyo linaonekana kuwalemea waasi, lakini limeshindwa kushinda kwenye vita hivi.

Umoja wa Ulaya kuijadili Syria

Katika hatua za karibuni kabisa kwenye jumuiya ya kimataifa dhidi ya mgogoro huu, Uingereza na Ufaransa zimetangaza kuanza kuushughulikia kivyao kwa kutishia kukiuka marufuku ya kuingiza silaha nchini Syria, endapo Umoja wa Ulaya hautaridhia kuviondoa vikwazo hivyo. Suala hilo linatarajiwa kujadiliwa leo katika siku ya mwisho ya kikao cha Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Hapo jana, Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema lengo lao ni kuwashawishi washirika wake kukubali kuondoa marufuku hiyo ya silaha kufikia mwezi Mei au hata mapema zaidi kwani suluhisho la kisiasa limefeli:

Upinzani nchini Syria umeyapokea vyema matamshi hayo ukisema ndiyo njia sahihi, ila utawala wa Assad na washirika wake Urusi wamesema hatua hiyo itakiuka sheria za kimataifa.

Marekani inaonekana kukubaliana na Uingereza na Ufaransa, ingawa haijabainisha kama itaunga mkono pendekezo la kuondoa marufuku hiyo, huku Ujerumani ikionekana kutokubaliana na hatua hiyo. Hapo jana Kansela Angela Merkel wa Ujerumani´alisema Umoja wa Ulaya unahitaji kutahadhari sana juu ya kuondolea mbali marufuku ya silaha dhidi ya Syria.

Mwandishi: Caro Robi/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef