1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yazidi kushinikizwa kuhusu silaza za kemikali

30 Aprili 2013

Syria inazidi kushinikizwa kufungua milango kwa wachunguzi wa silaha wa kimataifa ambapo marais wa Marekani na Urusi wamejadili suala hilo, huku Katibu Mkuu wa UN naye akiitaka serikali yake kutoa ushirikiano kamili.

https://p.dw.com/p/18PO5
Watu walioathirika na mashambulizi ya silaha zinazodaiwa kuwa na sumu.
Watu walioathirika na mashambulizi ya silaha zinazodaiwa kuwa na sumu.Picha: Reuters

Ikulu ya Marekani imesema jana Jumatatu kuwa rais Bashar al-Assad anapaswa kuwaruhusu wakaguzi wa umoja wa mataifa kuingia nchini Syria kuanza uchunguzi kubaini iwapo silaha za kemikali zilitumika. Msemaji wa Ikulu hiyo Jay Carney, aliwambia waandishi wa habari kuwa uhakika wa iwapo silaha silaha hizo zimetumika utapatikana kama timu ya wataalamu itaruhusiwa na utawala wa Assad kuingia ndani ya Syria.

Waokoaji wakimuoka majeruhi kutoka kwenye jengo lililoshambuliwa na makombora ya ndege za serikali ya Assad.
Waokoaji wakimuoka majeruhi kutoka kwenye jengo lililoshambuliwa na makombora ya ndege za serikali ya Assad.Picha: dpa/AP

Serikali inataka waasi tu ndiyo wachunguzwe

Serikali ya Syria iliuomba Umoja wa Mataifa mwezi uliopita kuanzisha uchunguzi, baada ya serikali hiyo kuwatuhumu waasi kwa kutumia silaha za kemikali wakati wa mapigano na vikosi vya serikali karibu na mji wa Aleppo. Lakini sasa imekataa kuwaruhusu wachunguzi wa umoja huo kuingia nchini Syria, kwa sababu wanataka kuchunguza pia vituo vya serikali. Waasi na wapinzani wanaituhumu serikali ya Assad kwa kutumia silaha za kemikali.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ukweli utabainika tu baada ya wachunguzi kuruhuisiwa kufanya kazi. "Uchunguzi wa ndani ya Syria kwenyewe ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kuweza kubaini ukweli na kuondoa mashaka yanayoghubika suala hili. Uchunguzi wa kuaminika na wa kina unahitaji kupata picha kamili kutoka katika maeneo ambako silaha za kemikali zinadaiwa kutumika," alisema Ban.

Rais Barack Obama alisema matumizi ya silaha za kemikali yataifanya nchi yake itafakari upya msimamo wake wa kutoingilia kijeshi nchini Syria, lakini akasisitiza kuwa Marekani lazima ipate ushahidi uliothibitishwa, kwamba shambulio lilifanyika kabla ya kutekeleza kitisho chake. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, naye alisisitiza kuwa ushahidi huo lazima uwe thabiti.

Rais Bashar al-Assad.
Rais Bashar al-Assad.Picha: REUTERS/Sana

Ban asema wachunguzi wako katika hatua muhimu

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon alisema timu ya wachunguzi imefikia hatua muhimu kwa sababu imekuwa ikikusanya taarifa ikiwa ni pamoja na kutoka Marekani, na kuzielezea taarifa hizo kuwa ni nzito. Timu ndogo ya kwanza inasubiri nchini Cyprus kuruhusiwa kuingia Syria.

Marekani na Uingereza zilisema wiki iliyopita kuwa kuna ushahidi unaozidi kuongezeka juu ya matumizi ya silaha za kemikali katika maeneo mbalimbali nchini Syria. Katika mkanda wa video uliowekwa kwenye mtandao, waasi wanadai ndege za serikali zimeangusha mabomu ya sumu, ambapo watu kadhaa wanaonekana wakisaidiwa kupumua kwa kutumia vifaa.

Maafisa wa Marekani wamebaini kamikali ya sarin, ambayo ina sumu kali na inaweza kusababisha kiharusi kwa haraka au kifo. Syria imekanusha madai hayo na kuyaita ya uwongo na uzushi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,ape
Mhariri: Daniel Gakuba