1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syriza kuunda serikali ya muungano Ugiriki

26 Januari 2015

Chama cha Ugiriki cha Syriza kinafanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano, baada ya kushinda katika uchaguzi wa bunge ambapo kiliahidi kujadiliana upya masharti ya uokozi na kanda inayotumia sarafu ya euro.

https://p.dw.com/p/1EQQW
Viongozi wa serikali ya Muungano Ugiriki, Tsipras na Kammenos
Viongozi wa serikali ya Muungano Ugiriki, Tsipras na KammenosPicha: AFP/Getty Images/L. Pitarakis

Kiongozi wa chama cha Syriza ambacho ni cha mrengo wa shoto, Alexis Tsipras, amekubaliana kuunda serikali ya muungano na kiongozi wa chama Huru cha Wagiriki cha mrengo wa kulia, Panos Kammenos, mshirika wake katika kupinga masharti ya kubana matumizi, ambacho tayari kimeonyesha nia ya kutaka kujiunga katika muungano.

Afisa mwandamizi wa Syriza, Dimitris Stratoulis, amekiambia kituo cha televisheni cha Mega, anaamini kwamba Tsipras atakuwa ameunda serikali ya muungano ifikapo leo jioni.

Uamuzi wa Tsipras kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano na chama Huru cha Wagiriki, kuliko chama cha mrengo wa kati cha Potami, umezusha wasiwasi mkubwa kwamba huenda makubaliano hayo yakawa na matokeo magumu dhidi ya wakopeshaji.

Afisa mipango wa uchumi wa chama cha Syriza, Giorgos Stathakis, amethibitisha leo kuwa serikali mpya haina mipango ya kukutana na wapatanishi wa Benki Kuu ya Ulaya, Shirika la Fedha Duniani-IMF na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na badala yake watatafuta kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali.

Wafuasi wa Syriza wakishangilia ushindi wao
Wafuasi wa Syriza wakishangilia ushindi waoPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Chama cha Syriza kimeshinda katika uchaguzi wa jana (25.01.2015), kwa asilimia 36.3 huku kikijinyakulia viti 149 katika bunge la Ugiriki lenye viti 300, ambapo kimepungukiwa viti viwili ili kuwa na wingi wa kutosha bungeni. Chama cha kihafidhina cha Waziri Mkuu anayeondoka madarakani Antonis Samaras, kimepata asilimia 27.8 huku chama cha Golden Dawn kikishika nafasi ya tatu baada ya kupata asilimia 6.28.

Tsipras asema umma umetoa maamuzi ya wazi

Akizungumza baada ya ushindi huo, Tsipras amesema umma wa Ugiriki umetoa maamuzi ya wazi. ''Ushindi wetu pia ni ushindi kwa watu wote wa Ulaya ambao wanapambana dhidi ya hatua kali za kubana matumizi ambazo zinaharibu mustakabali wa pamoja wa Ulaya, alisema Tsipras.''

Viongozi mbalimbali wameyazungumzia matokeo hayo ya uchaguzi ambapo Rais wa Bunge la Ulaya, Martin Schulz amesema tayari ameshazungumza na Tsipras kwa njia ya simu. Amesema hana wasiwasi iwapo Ugiriki inaweza ikajiondoa katika kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.

Waziri Mkuu wa Ugiriki anayeondoka madarakani, Antonis Samaras
Waziri Mkuu wa Ugiriki anayeondoka madarakani, Antonis SamarasPicha: Reuters/P.Tzamaros/FOSPHOTOS

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ameonya kuwa ushindi wa chama cha Syriza utaongeza matatizo ya kiuchumi barani Ulaya. Hata hivyo wanasiasa wa Uingereza wa mrengo wa shoto, wameufurahia ushindi huo.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa, amempongeza Tsipras kwa ushindi huo huku akielezea hamu yake ya kutaka kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Ugiriki na Ufaransa, katika kuimarisha utulivu wa sarafu ya Euro.

Hata hivyo, Ujerumani imesisitiza kuwa Ugiriki lazima iheshimu masharti ya mpango wa uokozi wa Euro bilioni 240, ambazo zilisaidia kuukoa uchumi wa nchi hiyo, lakini kwa masharti magumu ya kubana matumizi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFPE,DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga