1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa Mpya katika kesi ya Kiongozi wa zamani wa IMF; Dominique Strauss-Kahn,

1 Julai 2011

Aliyekuwa Mkuu shirika la Fedha Duniani, IMF, Dominique Strauss-Kahn, anatarajiwa kurudishwa mahakamani leo baada ya taarifa kuwa madai yanayomkabili ya kutaka kumbaka mhudumu wa kike wa hoteli, huenda sio kweli.

https://p.dw.com/p/11nFw
Dominique Strauss-Kahn, akitiwa nguvuni baada ya mhuduni wa hoteli, kudai alitaka kumbakaPicha: dapd

Kuna uwezekano kwa kufutwa kesi inayomkabili, kiongozi huyo wa zamani wa shirika hilo la fedha duniani, baada ya taarifa mpya kutoka vyanzo vya ndani, karibu na kesi hiyo,kusema waendesha mashtaka hawaamini madai ya mhudumu huyo wa hoteli, mzaliwa wa Guinea.

Gazeti la New York Times jana lilizinukuu vyanzo viwili vya habari karibu na kesi hiyo vikisema kuwa waendesha mashtaka hawaamini madai ya mhudumu huyo, na kwamba wanadhani mhudumu huyo amekuwa akiwadanganya.

Maofisa hao wamesema ndani ya siku moja baada ya kutoa madai hayo, mhudumu huyo alirekodiwa akijadili manufaa ya kuendelea na madai hayo ya ubakaji, kwenye simu na mwanaume aliyeko jela kwa kosa la kukamatwa na kilo 180 za bangi.

Dominique Strauss-Kahn Gericht IWF 19.05.
Mkuu wa zamani, IMF; Dominique Strauss-Kahn, (kulia) akinena jambo na wakili wake.Picha: AP

Gazeti hilo limesema mwanaume huyo ni miongoni mwa watu walioweka fedha katika akaunti ya mhudumu huyo, jumla ya dola za kimarekani 100,000 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Miongoni mwa mambo yaliyogunduliwa kuhusu mhudumu huyo, mwenye miaka 32, pia ni masuala ya kuomba hifadhi na kwamba kuna uwezekano wa mhudumu huyo kuwa na mahusiano ya kihalifu, ikiwemo madawa ya kulevya na uhamishaji wa fedha ambazo sio halali.

Inasemakana kuwa matokeo ya kusikilizwa kesi hiyo leo, huenda yakalegeza masharti ya dhamana yaliyowekwa dhidi ya Strauss-Kahn, na kumpa uhuru wa kutembea nchini Marekani.

Wanasheria pia wanajadili kutupilia nje madai hayo ya kutaka kumbaka mhudumu huyo wa hoteli.

Strauss-Kahn, ambaye alikuwa pia waziri wa zamani wa fedha wa Ufaransa, na aliyetarajiwa kutangaza nia yake kugombea nafasi ya urais nchini humu mwaka ujao, alitarajiwa kurudi mahakamani tarehe 18 mwezi huu.

Nchini Ufaransa leo, taarifa hizo zimeleta matumaini kwa chama cha upinzani cha Kisosholisti kuwa Strauss-Kahnn anaweza kurudi nchini humo na kupambana na rais Nicolas Sarkozy kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya urais mwakani.

Anne Sinclair Ehefrau von Dominique Strauss-Kahn
l Dominique Strauss-Kahn, akiwa na mke wake Anne Sinclair.Picha: dapd

Jean-Marie Le Guen, mbunge wa kisocsholisti, na mtu wa karibu wa kiongozi huyo wa zamani wa IMF, amasema Strauss-Kahn haepukiki katika siasa za Ufaransa.

Amesema wale wote waliodhani kuwa Strauss-Kahn ametoka kwenye siasa za Ufaransa sasa wahesabu kuwa anarudi na ataweza kutembea na kuwaangalia machoni.

Le Guen amesema Strauss-Kahn ana uzoefu mkubwa, malengo na uwezo wa kushinda, na itakuwa ni nguvu mpya katika chama hicho cha Kisosholisti.

Mwandishi: Rose Athumani/AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman